Home Sports NABI AWAPA MAAGIZO WACHEZAJI WAKE

NABI AWAPA MAAGIZO WACHEZAJI WAKE

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ni kama amewajaza upepo washambuliaji wa timu hiyo akiwemo Fiston Mayele kwa kuwa waambia kuwa wanauwezo mkubwa wa kufunga mabao mengi katika kila mchezo ikiwa tu wataamua kuzitumia vizuri nafasi wanazopata.

 

Nabi ametoa kauli hiyo baada ya mazoezi ya juzi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam unaotarajia kupigwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

 

Kauli ya kocha huyo imetokana na uchache wa mabao yaliyofungwa na safu ya ushambuliaji tangu kuanza ligi msimu huu ambapo kwenye mechi tatu, safu hiyo inayoongozwa na Fiston Mayele, Harietier Makambo na Yusuph Athuman imefunga bao moja pekee ambalo mfungaji wake ni Mayele.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Nabi alisema kuwa washambuliaji wake wana kila sababu ya kuhakikisha wanafunga mabao ya kutosha kwa kuwa uwezo wa kufanya hivyo wanao kutokana na nafasi wanazokosa katika mechi ambazo wamecheza mpaka sasa.

 

“Bado safu ya ushambuliaji haijafanya kile ambacho tunachokitarajia ingawa ndiyo tunaenda kucheza mechi ya nne dhidi ya Azam lakini suala la kufunga linahitaji umakini hasa kwa wafungaji wenyewe katika kila mchezo,
kufunga mabao mengi ni 
ishara ya kuonyesha kitu gani ambacho tunahitaji msimu huu.

 

“Matumaini yetu ni kushinda licha ya kutambua ugumu na ubora wa wapinzani wetu lakini kikubwa ambacho tunahitaji kuona ni kwamba tunapata matokeo, tumeanza ligi vizuri lakini bado tunahitaji kuboresha safu ya ushambuliaji ili kufunga mabao mengi katika kila mchezo ambao upo mbele yetu,” alisema Nabi.

Previous articleHUKUMU YA MORRISON NA CAS KUTOLEWA
Next articleOLE BADO YUPO SANA MANCHESTER UNITED