KLABU ya Paris Saint Germain ya nchini Ufaransa imemtimua kazi kocha wake raia wa Argentina Mauricio Pochettino ikiwa ni baada ya kuwa klabuni hapo kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.
Pochettino ambaye amewahi kuwa kocha wa Totenham Hotspurs ya nchini Uingereza ametimuliwa kibaruani baada ya kutokuwa na matokeo mazuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya licha ya kuwa na kikosi kilichosheheni nyota wa kiwango cha dunia kama vile Lionel Messi, Neymar Jr pamoja na Kylian Mbappe.
Licha ya kutimuliwa Pochettino amefanikiwa kuchukua kombe la Ligi Kuu ya Ufaransa maarufu kama Ligue 1 ndani ya msimu wake mmoja ambao ulitawaliwa na PSG kwa takribani kipindi chote cha msimu.
Kumekuwa na taarifa kuwa moja ya mambo yaliyosababisha kutimuliwa kwa Pochettino ni pamoja na kushindwa kuwaongoza wachezaji wenye majina makubwa kama Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe ambao wengi wao wana mafanikio makubwa kuliko kocha.
Kwa upande mwingine PSG imemtangaza kocha wa zamani wa Klabu ya Nice ya Ufaransa Christophe Galtier kama mrithi wa Pochettino, raia huyo wa Ufaransa mwenye miaka 55 amelamba mkataba wa miaka miwili wa kuinoa miamba hiyo ya nchini Ufaransa.
Mara baada ya kuteuliwa Galtier amesema:“Najisikia faraja kujiunga na Paris Saint Germain, ningependa kumshukuru Mwenyekiti Nasser Al- Khelaifi, Mshauri wa masuala Luis Campos pamoja na klabu kwa Imani yao kwangu.”
PSG inatarajiwa kuwa na msimu mzuri kutokana na kuweza kuzuia baadhi ya nyota wao kutoondoka klabuni hapo akiwemo Kylian Mbappe ambaye alikuwa anapigiwa chapuo la kutimkia klabu ya Reala Madrid.