INARIPOTIWA kuwa straika, Cesar Manzoki raia wa Afrika Kati mwenye uraia wa DR Congo amewafanyia umafia wa kutisha mabosi wa Simba ikiwa ni muda mchache kabla ya kutua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini mkataba na badala yake akaelekea DR Congo huku mabosi wa Yanga wakitajwa kwenye umafia huo.
Manzoki ambaye ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira akiwa anatumia miguu yote katika kupiga mashuti pamoja uwezo mkubwa wa kuruka mipira ya vichwa, safari yake ya soka ilianzia katika Klabu ya AS Dauphins Nours ya DR Congo ambayo alicheza kutoka 2012 hadi 2017, kisha akatimkia AS Miniema Union ambayo alicheza kwa msimu mmoja kabla ya kutua AS Vita mwaka 2018 hadi 2020 alipojiunga na Vipers ya Uganda.
Manzoki ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda msimu huu wa 2021/22 akitupia mabao 18, pia katika tuzo zilizotelewa wikiendi iliyopita, mshambuliaji huyo aliweka rekodi ya kuchukua tuzo tano ikiwemo ya mfungaji bora, mchezaji bora, mshambuliaji bora, mchezeshaji bora na pamoja na kuingia kwenye kikosi bora cha msimu.
Ikumbukwe kabla ya Simba kumfuata mshambulaji huyo, Yanga walikuwa wa kwanza kumfuata na kufanya naye mazungumzo lakini wakamkaushia ila baada ya kusikia Simba wanakaribia kumsajili wakarudisha majeshi kwa kuingilia kati dili hilo.
Chanzo cha kuaminika kilisema kuwa, baada ya Simba kukamilisha mazungumzo na nyota huyo, wakakubaliana atue nchini ili wamalizane na kumtangaza baada ya mechi za kimataifa ambapo yeye alikuwa akiitumikia Afrika ya Kati.
Kiliendelea kusema kuwa, Manzoki alipomaliza majukumu yake alipanda ndege na kuelekea DR Congo kwa maelekezo ya mabosi wa Yanga ambao wameamua kuwafanyia undava wapinzani wao, Simba huku wakidaiwa kumtaka mshambuliaji huyo azime simu wakati wakiwa wanashughulikia mchakato wa kumsajili.
“Usajili wa Manzoki Simba una danadana nyingi, walikubaliana baada ya kumalizika kwa zile mechi za kimataifa tu basi aje Dar ili wamalizane na kisha wamtambulishe lakini yeye alipitiliza DR Congo, baada ya hapo hakupatikana kwenye simu yake,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kuinyaka taarifa hiyo, Championi lilimtafuta mmoja wa mawakala wake kutoka Kampuni ya Agbeve Kspots Management, jana mchana lakini alidai yupo kwenye kikao na atakapokuwa tayari ataweka wazi kila kitu.