SIMBA NOMA YATUMIA UJANJA KUMNASA KIUNGO FUNDI

UNAAMBIWA pamoja na Wydad Casablanca na Raja Casablanca zote za Morocco kuhitaji saini ya kiungo raia wa Guinea, Morlaye Sylla, Simba SC imetumia ujanja wa kwenda kuzungumza na familia ya nyota huyo.

Sylla msimu huu amekichakaza vilivyo ndani ya kikosi cha Horoya AC ya Guinea, ambayo alijiunga nayo Julai Mosi 2019, kwa mkataba wa miaka mitatu, akitokea CO de Coyah ya nchini humo.

Chanzo chetu kutoka Simba, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, pamoja na miamba hiyo ya Morocco, kudaiwa kuingilia usajili huo, Simba wamefanya umafia kwa kuzungumza na familia yake ambayo imeonesha matumaini makubwa ya kukamilisha dili lake.

“Kusema kweli kwa sasa suala la usajili kwetu limekuwa ni sehemu ya vita kali, maana kila mchezaji tunayemuhitaji utakuta kuna timu zingine kama tatu kubwa nazo zinamuhitaji, hivyo inatupa ugumu sana kukamilisha dili hizo.

“Jambo la kujivunia kwetu kwa sasa ni kuwa, tumefanikiwa sana kuwanasa baadhi ya wachezaji wa nje kufuatia ule umafia tuliouzoea kutokea hapa nchini, hivyo utaona hata sasa tumelazimika kuzizunguka Wydad na Raja ili tu tufanikishe saini ya Morlaye Sylla raia wa Guinea.

“Kama hakutatokea mabadiliko yoyote basi siku hizi mbili utamuona hapa nchini, japo usajili wake umekuwa ukiingiliana sana na ujio wa kocha ambaye naye tumemwekea dau kubwa,” kilisema chanzo hicho.