M-BET YAIPIGA TAFU TASWA SC

KAMPUNI ya michezo ya kubahatisha nchini, M-Bet Tanzania imeisaidia vifaa vya michezo timu ya Waandishi wa Habari za michezo nchini, Taswa SC kwa ajili kutimika katika shughuli mbalimbali za michezo nchini.

Vifaa hivyo ni jezi na mpira ambapo Meneja Masoko wa M-Bet Tanzania, Allen Mushi amesema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuvutiwa na mwenendo wa Taswa SC katika mechi zake mbalimbali.

Taswa SC inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Bunge SC) Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mbali ya mechi hiyo, timu ya netiboli ya Bunge (Bunge Queens) nayo watapambana na timu ya Taswa Queens.

Kwa mujibu wa Mushi, M-Bet Tanzania inajisikia fahari kubwa kuisaidia Taswa SC katika shughuli zake na hasa katika mchezo wao wa Jumamosi.

“Ni faraja na fahari kubwa kuisaidia timu ya Taswa SC ili kufanikisha kucheza mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa na ushindani pia. M-Bet itaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za michezo na sekta nyingine ili kusaidia ustawi wake,” alisema Mushi.

Mwenyekiti wa Taswa SC, Majuto Omary aliipongeza Kampuni ya M-Bet Tanzania kwa kuwasaidia na kuwaahidi kutowaangusha katika mechi hiyo na nyinginezo zitakazofuata.

Majuto amesema kuwa bado wanachangamoto nyingi lakini kutokana na mshikamano baina yao, wameweza kuzikabili na kusonga mbele.

 “Huu ni msaada mkubwa sana kwetu na utafungua njia kwa makampuni mengine kutusaidia. Klabu ina mahitaji mengi na tunaamini taasisi, kampuni na watu binafsi watatusaidia,” alisema Majuto.

Kwenye timu hiyo kuna nyota bora wa muda wote ambaye ni kiungo Wilert Moland huyu ni nahodha pia wa timu ya Global FC.