Home Sports HIVI NDIVYO PABLO ATAKAVYOFANYA USAJILI SIMBA

HIVI NDIVYO PABLO ATAKAVYOFANYA USAJILI SIMBA

UONGOZI wa Simba umesema kuwa, kocha wao mpya atatumia ripoti ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mhispania, Pablo Franco kwa ajili ya kufanya usajili wa msimu ujao.

Simba tayari imeanza usajili wa kimyakimya huku wakimsubiria kocha mpya atakayetangazwa hivi karibuni akija kuchukua mikoba ya Pablo aliyetimuliwa Mei, mwaka huu.

Timu hiyo ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs, Stuart William Baxter, kwa ajili ya kuinoa timu hiyo.

 Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mapendekezo ya usajili aliyoyatoa Pablo kwa ajili ya msimu ujao, ndiyo watakayofanyia kazi kuhakikisha wanafanya usajili mzuri.

Ally alisema Pablo kabla ya kuondoka aliwasilisha ripoti ya usajili ambayo imetoa mapendekezo ya wachezaji wapya wa kusajiliwa na kuachwa kwa ajili ya msimu ujao.

Aliongeza kuwa, ripoti hiyo ya usajili anatarajiwa kukabidhiwa kocha mpya mara baada ya kutua nchini na kusaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho.

“Kabla ya ligi kumalizika, kocha mpya atakuwa amewasili nchini tayari kwa ajili ya kutambulishwa mara baada ya kusaini mkataba.

“Kocha huyo mara baada ya kusaini mkataba atakabidhiwa ripoti ya usajili aliyoikabidhi Pablo kwa wachezaji aliopanga kuwasajili na wale wa kuwaacha.

“Ngumu kwa kocha mpya kufanya usajili bila ya muongozo kwani hakuwa na timu, itakuwa ngumu kwake kujua upungufu wa timu, hivyo ripoti ya Pablo ndiyo itakayotumika kufanya usajili, lakini pia kocha huyo atapewa nafasi ya kufanya usajili kwa baadhi ya nafasi,” amesema Ally.

Previous articleM-BET YAIPIGA TAFU TASWA SC
Next articleYANGA:UBINGWA ASILIMIA 99