AZAM FC WANASUBIRI TAARIFA KUTOKA BODI YA LIGI

 UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa hauna tatizo ikiwa watapewa taarifa kwamba mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting utapangiwa tarehe nyingine kutokana na taarifa kueeleza kuwa Ruvu Shooting wameomba iwe hivyo.

Ruvu Shooting kupitia kwa Ofisa Habari wao, Masau Bwire ameweka wazi kuwa wameiandikia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania,(TPLB) barua ya kuomba kupewa muda wa kupumzika kwa kuwa watatumia muda mwingi kwenye safari wakitokea Kagera.

Ikumbukwe kwamba Ruvu Shooting walikuwa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba na kukamilika kwa tasa ya bila kufungana usiku.

Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa hawajapata taarifa yoyote kutoka Bodi ya Ligi inayozungumzia mechi yao kupangiwa muda mwingine.

“Hadi sasa hatujapata taarifa yoyote kutoka Bodi ya Ligi kama maombi ya Ruvu Shooting yamekubaliwa ama hayajakubaliwa ila tutajulishwa endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote.

“Kwa upande wetu sisi hatuna tatizo lolote endapo mechi itasongezwa mbele kwa sababu ni haki yao ,(Ruvu Shooting) kupata muda wa kupumzika ili kujiandaa vema.”.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa leo Mei 24 Uwanja wa Mabatini saa 10:00 jioni.

Chanzo:Spoti Xtra