YANGA YAGOMEA SARE TENA KWENYE LIGI

MARA baada ya kupata suluhu katika michezo mitatu mfululizo kwenye ligi kuu, benchi la ufundi la timu hiyo, limesema kuwa kwa sasa inatosha na litapambana kuhakikisha kuwa timu hiyo inapata ushindi katika michezo inayofuata na kuendeleza matumaini ya ubingwa msimu huu.

Yanga imeshindwa kupata ushindi wala kufunga bao katika michezo mitatu iliyopita mfululizo dhidi ya Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons.

 Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa matokeo ambayo wameyapata katika michezo iliyopita yamewasikitisha na watapambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo ujao ili kuendelea na mbio za kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu

“Tunatakiwa kuhakikisha tunashinda katika michezo yetu ijayo, matokeo ya michezo iliyopita sio mazuri kwetu na tumeumia kuona tumepata matokeo haya, sio wachezaji wala viongozi wote tumeumia sana.

“Mashabiki pia lazima watakuwa wanaumia na haya matokeo na muhimu kwa sasa ni matayarisho ya michezo ijayo ambapo tunatakiwa kufanya vizuri zaidi kwa kupata ushindi ili kuendelea kuwa karibu na ubingwa,” amesema kocha huyo.

Mchezo ujao wa Yanga ni dhidi ya Dodoma Jiji ambao unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri.