YANGA imeonekana kupania kufanya usajili bora utakaokuwa tishio kimataifa baada ya kumfuata mshambuliaji wa US Gendarmarie ya nchini Niger, Victorien Adebayor ambaye imemuwekea Sh 250Mil ili kuinasa saini yake.
Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kumfuata mshambuliaji huyo anayecheza kwa mkopo Gendarmarie ambaye anamilikiwa na Klabu ya HB Køge inayocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Denmark.
Timu hizo zote zimemuona mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 katika Kombe la Shirikisho Afrika akiwa anaichezea Gendarmerie.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, amesema kuwa wao wamefuata taratibu za usajili kwa kumfuata meneja wa mshambuliaji huyo na kufanya naye mazungumzo mazuri yaliyofikia muafaka mzuri.
Bosi huyo alisema kuwa meneja wa mchezaji huyo ameonekana kushawishika na Yanga baada ya kuwaona Simba walioweka dau la Sh 200Mil ili waipate saini ya nyota na kuingia mitini baada ya kushindwana katika fedha hiyo ya usajili.
Aliongeza kuwa baada ya Simba kuingia mitini, mabosi wa Yanga wenyewe walikubali kuongeza dau la usajili kutoka Sh 200Mil na kufikia 250Mil ili wawazidi watani wao wa Msimbazi.
“Meneja amewaona hawapo siriazi na Adebayor katika kumsajili, ni baada ya kushindwa kurudi tena kwake kwa ajili ya mazungumzo baada ya kutajiwa dau la usajili wanalolitaka ambalo ni Sh 200Mil.
“Yanga walionekana kushtukia dili na haraka walimfuata meneja wa mshambuliaji huyo kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ambayo yamefikia muafaka mzuri kwa kukubali kutoa dau la Sh 250Mil ili waipate saini ya Adebayor.
“Hivyo kama mambo yatakwenda vizuri kati ya meneja na Yanga, basi upo uwezekano mkubwa wa Adebayor kutua Yanga ambayo ameonekana kuifuatilia kwa karibu na kushawishika na historia ya timu hiyo kongwe na kubwa Afrika,” alisema bosi huyo.
Yanga kwa kupitia kwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni aliliambia gazeti hili: “Tumepanga kuvunja benki kufanya usajili utakaokuwa bora na kuleta ushindani kimataifa.
“Hatutafanya masihara katika usajili wetu huu wa msimu ujao, kikubwa tunataka kuirudisha Yanga katika hadhi na ubora wake.”
Hayo yamekuja wiki chache tangu Simba kupitia kwa Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, kusema kuwa, Adebayor atakuwa mchezaji wao msimu ujao kwa kuwa wameshafikia makubaliano naye kwa asilimia kubwa.
Simba iliwahi kupigwa bao maarufu na Yanga katika usajili, wakati mwenyekiti wa Simba wa enzi zile, Ismail Rage, aliposafiri hadi Rwanda kumsajili Mbuyu Twite akapiga naye picha akijinasibu kuwa wameshamalizana naye, lakini siku chache baadaye akasaini Yanga na alipotua nchini mashabiki wakamvisha jezi ya njano iliyoandikwa mgongoni ‘Rage!”