ANAANDIKA Saleh Jembe
Ukimsikiliza kocha huyu wa Orlando Pirates, unaweza kusikitika sana na leo unaona ndiye amekuwa gumzo kwa kuwa sisi Watanzania ni wepesi kuamini ya kuambiwa kuliko tunayoona.
Kawaida ya watu wa Afrika Kusini ni kulalamika kila jambo hata kama hawana uthibitisho. mfano, kocha huyu analalamikia VAR haikufanya kazi, tena anawalalamikia Simba na sisi tumeendelea kuaminishwa na wengine, eti ni kweli haikufanya kazi!
Simba wanahusika na VAR, tunajua sote ni Caf ndio wahusika ndio wenye mashindano yao, vipi awalalamikie Simba? Nani ana uthibitisho VAR haikufanya kazi?
If hakuna sasa kwa nini tunaamini na macho yanatuonyesha mwamuzi alifanya mawasiliano na watu wa VAR na unaona aliwaambia wachezaji wa Orlando kwa ishara kuwa watu wa VAR ndio wamethibitisha baada ya kupata sekunde kadhaa za kuwasiliana nao.
Achana na hiyo, kocha anasema hawajatendewa haki au walifanyiwa vitendo visivyo sijui kuanzia hotelini. Simba wanahusikaje na hoteli waliyotafuta na kufikia wao? Kama ni barabarani ni vitendo vipi, mbona hawasemi?
Ukiwa makini utagundua ni mwendelezo wa propaganda ya kipuuzi kabisa ambayo inatokana na tabia za watu wa Afrika Kusini kuamini wao ni kila kitu na kulalamikaaaa ndio maisha. Angalia, kocha analalamika lakini hana hata mfano mmoja wa matukio waliyifanyiwa.
Mwambieni kocha aache siasa kwenye mpira, suala la WE ARE AFRICAN wala lisiwe kisingizio cha kila kitu wanaposhindwa na mumkumbushe.
Simba haina mwamuzi, awasiliane na Caf Simba haina uwezo wa kujipa au kuwanyima penalty, awasiliane na Caf Simba haikuwapangia hoteli, haina uwezo wa kwenda kuwanyanyasa hotelini
Nawakumbusha, hawa Orlando walitengeneza propaganda kuwa Simba wanahonga waamuzi, wakasingizia moja ya gazeti lao kufanya mahojiano na Abdi Banda ambaye alipinga na kuniambia hakuwa amezungumza na mwandishi yoyote wa hapa au Afrika Kusini kwa muda mrefu.
Lakini walisambaza mtandaoni kutaka kuonyesha Simba watahonga, leo wanalalamikia kila kitu.
Wamefungwa, zamu ya Simba kwenda kupambana na ikiwezekana itakuwa bora, ikishindikana ndio mpira lakini vizuri nawe jifunze, si kila KINACHOZUNGUMZWA KWA KINGEREZA NI KITAMU NA MJADALA SAHIHI.