KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kinatarajiwa kushuka uwanjani Aprili 23 kusaka pointi tatu dhidi ya Namungo FC.
Ni mchezo wa ligi ambapo utakuwa ni wa mzunguko wa pili baada ya ule wa awali walipokutana Uwanja wa Ilulu ubao kusoma Namungo 1-1 Yanga.
Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mechi zote watakazocheza na kikubwa wanahitaji pointi tatu.
“Tunaua mchezo wetu dhidi Namungo utakuwa na ushindani mkubwa, wapinzani wetu tunawaheshimu hivyo ambacho tunakifanya ni maandalizi mazuri.
“Wachezaji wapo tayari na kila kitu kinakwenda sawa hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi ili kuweza kuona namna gani tunapata matokeo,” amesema.
Miongoni mwa viungo wa kazi ambao wamekuwa wakitumika kwenye namba tofauti ni pamoja na Farid Mussa ambaye ameweza kuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza kwenye mechi za hivi karibuni.