KINYONGE kabisa wawakilishi pekee katika mashindano ya kimataifa Simba wanakwenda katika Kombe la Shirikisho baada ya Oktoba 24 kutolewa kizembe Uwanja wa Mkapa kwa kufungwa mabao matatu ya ajabu wakiwa nyumbani.
Ni maumivu kwa mashabiki wa Simba,viongozi pamoja na wachezaji kwa kukosa nafasi ya kutinga hatua ya makundi, leo tunaangazia mabmbo 7 ambayo yaliifanya Simba kufungashiwa virago Ligi ya Mabingwa Afrika:-
Kuridhika
Ushindi wa mabao 2-0 nchini Botswana ambapo mabao yalipatikana kupitia kwa John Bocco na Taddeo Lwanga kukawafanya Simba kuamini kwamba kazi imeisha.
Hata walipofungwa mabao mawili Uwanja wa Mkapa bado walionekana kuamini kwamba mchezo umekwisha walikuja kushtuka walipofungwa bao la tatu ila kwa kuwa walikuwa wameshamaliza mchezo akilini mwao na ubao ukakamilika Simba 1-3 Jwaneng Galaxy.
Umakini mdogo
Kushindwa kutumia nafasi ambazo walizipata kwene mchezo huo, kona 8 ambazo walipata zote hazikuweza kuwapa matunda kama ilivyokuwa Uwanja wa Taifa wa Botswana.
Pia wachezaji wake ikiwa ni pamoja na Bernard Morrison, Peter Banda na Rarry Bwalya ambaye alifunga bao pekee kwa Simba walikuwa na nafasi za dhahabu ila walishindwa kuzitumia pamoja na beki Shomari Kapombe ambaye alikuwa akitegemewa kumwaga majalo kati.
Dharau
Hakuna mchezaji wala kiongozi wa Simba ambaye alikuwa anaamini kwamba kuna ishu ya kufungwa Uwanja wa Mkapa licha ya kwamba wote walikuwa na dakika 90 hivyo ilikuwa ni dharau jambo ambalo ni kosa.
Tatizo la kuamini kwamba wapinzani wao hawana rekodi kubwa kimataifa hasa ukizingatia ni timu ambayo ilianzishwa 2015 nchini Botswana na 2018 iliweza kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kuishia hatua ya awali hivyo hawakuwa na rekodi nzuri kimataifa wameibukia kwa Mkapa na kutinga hatua ya makundi.
Kauli ya kocha wa Jwaneng Galaxy
Kocha Mkuu wa Jwaneng Galaxy, Lesika Keatlhotswe siku moja kabla ya mechi alieleza kuwa wamekuja kukamilisha ratiba wanaona Simba imeshafuzu hatua ya makundi wao akili yao ni kujiandaa na Ligi Kuu ya Botswana inayoanza hivi karibuni.Hapa Jwaneng walitumia akili kuwadumaza wapinzani wao.
Baada ya ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 1-3 Jwaneng Galaxy, kocha huyo alibainisha kuwa wapinzani wao Simba ni wazuri kwenye mipira iliyokufa halafu mabeki ni wabovu kwenye kuzuia mipira iliyokufa.
Rekodi ya Uwanja wa Mkapa kutofungwa
Simba walikuwa na rekodi tamu Uwanja wa Mkapa ambapo kwenye mechi kubwa zote za Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni ngumu kufungwa na wakaamini kwamba itakuwa hivyo.
Miongoni mwa timu kubwa ambazo zilionja joto ya jiwe ni pamoja na AS Vita, Al Ahly ambayo kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa kwa misimu tofauti haijawahi kupata ushindi zaidi ya kutunguliwa bao mojamoja.
Pia mchezo wao wa hivi karibuni dhidi ya Kaizer Chiefs uliweza kuwa na ushindani mkubwa na mwisho wa siku Simba ilishinda mabao 3-0 ila ilikwama kutinga hatua ya nusu fainali kwa sababu ilikuwa imepoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 4-0 ugenini.
Luis na Chama
Viungo hawa wawili walikuwa ni mhimili wa Simba ambapo Clatous Chama alitengeneza jumla ya pasi 15 na kufunga mabao 8 huku Luis Miquissone akifunga mabao 9 na kutengeneza pasi 10 hivyo wote wawili kuondoka kwa wakati mmoja kumeiyumbisha Simba.
Wachezaji kutokuwa tayari
Inaonekana kwamba wachezaji ambao wapo Simba kwa sasa hawajakomaa katika ushindani pamoja na kuwa na majeruhi wengi.
Kijana kama Peter Banda ni mzuri lakini anahitaji uzoefu, kukosekana kwa Chris Mugalu, Jonas Mkude,Pape Osmane, Mzamiru Yassin ambao hawa hawapo fiti ni tatizo ambalo linaitesa Simba kwa sasa.