AZAM FC BADO HAIJAFIKA KWENYE UBORA WENYEWE

KOCHA Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Abdi Hamid Moalin, amesema bado hajaipata Azam anayoitaka na ubora wa kikosi chake kwa sasa hauzidi asilimia 65 hivyo bado jambo lao ni kusaka uimara kwa asilimia kubwa.

Moalin amefunguka kuwa kuna levo ya ubora ambayo anahitaji kuiona kwenye timu yake, jambo ambalo bado analifanyia kazi kwa sasa na atafanikiwa muda siyo mwingi.

“Timu inapata matokeo ya ushindi mfululizo, ila kwetu bado hatujafikia kwenye kiwango ambacho tunahitaji timu icheze na idumu kwenye ubora huo. Nafikiri (kwa sasa) ni kama asilimia ni 55 au 65 tu.

“Kila kitu kinakwenda sawa naona wachezaji wanapenda kazi yao na hii ni furaha kwetu kupata matokeo ambayo tunahitaji, ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji ushindi,” amesema.

Azam imeshinda mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara, haijapoteza mechi yoyote tangu ifungwe na Simba 2-1 siku ya Mwaka mpya wa 2022.

Mchezo ujao kwa Azam FC ni dhidi ya Biashara United unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Karume,Mara itakuwa ni Februari 22.