Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, kocha huyo raia wa Argentina anaonekana kuwa chaguo linalofaa kurejesha makali ya Manchester United kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu England, uwezo wa kukuza vipaji na namna anavyoweza kujenga mshikamano ndani ya kikosi.
Pochettino, ambaye amewahi kuzifundisha Tottenham Hotspur na Chelsea, anatajwa kuwa tayari kukubali changamoto ya kuiongoza Manchester United endapo klabu hiyo itaamua kuachana na Carrick.
Zifuatazo ni sababu tano zinazomfanya Pochettino kuonekana kuwa chaguo sahihi kwa miamba hiyo ya Old Trafford.
1. UWEZO WA KUKUZA NA KUINUA KIWANGO CHA WACHEZAJI
Moja ya sifa kubwa za Pochettino ni uwezo wake wa kuboresha kiwango cha wachezaji na kuwasaidia kufikia uwezo wao mkubwa.
Kocha huyo amewahi kufanya kazi na nyota kama Harry Kane, Son Heung-min, Dele Alli na Cole Palmer, ambao walinufaika na mbinu zake za ufundishaji.
Palmer aliwahi kueleza kuwa Pochettino alimpa uhuru wa kucheza kwa ubunifu na kumsaidia kujiamini zaidi ndani na nje ya uwanja.
Manchester United ina wachezaji vijana wenye vipaji kama Kobbie Mainoo, Leny Yoro, Ayden Heaven, Patrick Dorgu na Amad Diallo ambao wanaweza kunufaika na uzoefu wa kocha huyo.
2. UWEZO WA KUJENGA UMOJA NA FAMILIA NDANI YA VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO
Manchester United imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kukosa mshikamano wa kutosha ndani ya kikosi katika kipindi cha baada ya Sir Alex Ferguson.
Hata hivyo, Pochettino anasifika kwa kujenga mazingira mazuri ya kazi na kuimarisha mahusiano kati ya wachezaji na benchi la ufundi.
Dele Alli aliwahi kumuelezea kocha huyo kuwa na tabia za kimalezi, akisema alikuwa mtu aliyekuwa tayari kuwashauri wachezaji hata kuhusu mambo yao binafsi.
Harry Kane naye aliwahi kueleza namna Pochettino alivyoweza kujenga mazingira ya kifamilia na undugu miongoni mwa wachezaji wa Tottenham.
Uwezo huo unaweza kuwa muhimu kwa Manchester United katika kurejesha umoja na nidhamu ndani ya kikosi.
3. UZOEFU WA KUIFUMUA TIMU ILIYOPO KATIKA HALI NGUMU
Pochettino amewahi kukabidhiwa timu zilizokuwa na changamoto kubwa na kufanikiwa kuzibadilisha kuwa washindani wa juu.
Akiwa Tottenham, alikuta klabu iliyokuwa na changamoto za ndani baada ya kipindi kigumu cha Tim Sherwood, lakini aliweza kujenga kikosi kilichoshindania ubingwa wa Premier League na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019.
Pia, alipokuwa Chelsea, alikabiliana na mwanzo mgumu kabla ya kuimarisha mwenendo wa timu na kuisaidia kumaliza katika nafasi za kushiriki michuano ya Ulaya.
Uzoefu huo unatajwa kuwa muhimu kwa Manchester United ambayo inahitaji kurejesha ushindani wake dhidi ya timu kubwa za England na Ulaya.
4. MAHUSIANO MAZURI NA VYOMBO VYA HABARI
Kazi ya kuifundisha Manchester United inaambatana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki, vyombo vya habari na wachezaji wa zamani wa klabu hiyo.
Pochettino anaonekana kuwa na uwezo wa kukabiliana na mazingira hayo kutokana na mahusiano yake mazuri na wanahabari wa Uingereza.
Pia amewahi kushiriki katika vipindi vya mijadala ya soka pamoja na Gary Neville, mmoja wa wachambuzi wenye ushawishi mkubwa katika soka la England.
Neville aliwahi kumtaja Pochettino miongoni mwa makocha wanaoweza kuiongoza Manchester United kutokana na uwezo wake wa kusimamia vyumba vya kubadilishia nguo, kushughulika na wamiliki wa klabu na kuleta aina ya soka inayowafurahisha mashabiki.
5. KUMFUFUA MARCUS RASHFORD
Mshambuliaji Marcus Rashford ni miongoni mwa wachezaji ambao Pochettino anaweza kuwasaidia kurejesha kiwango chao bora.
Rashford, ambaye amefunga mabao 138 katika kikosi cha kwanza cha Manchester United, amekuwa na wakati mgumu kurejesha makali yake licha ya kuwa na kipaji kikubwa.
Kwa mujibu wa The Sun, Rashford hajawa na mchango mkubwa katika mwanzo wa msimu wa 2026/27, jambo linaloibua maswali kuhusu namna bora ya kutumia uwezo wake.
Pochettino aliwahi kueleza mwaka 2022 kuwa amekuwa akimkubali Rashford na anaamini kuwa mshambuliaji huyo anahitaji kujiamini zaidi ili kufikia kiwango cha juu.
Kauli hiyo inaongeza matumaini kuwa endapo atapewa nafasi ya kuifundisha Manchester United, anaweza kuwa na mchango mkubwa katika kurejesha makali ya Rashford.
HATMA YA CARRICK YASUBIRIWA
Kwa sasa, mustakabali wa Michael Carrick katika benchi la Manchester United unaendelea kuwa gumzo, huku Pochettino akitajwa kama mmoja wa wagombea wanaoweza kuchukua nafasi yake.
Uzoefu wake katika Premier League, uwezo wa kukuza vijana na kujenga mshikamano wa kikosi ni miongoni mwa mambo yanayomfanya aonekane kuwa chaguo lenye mvuto kwa viongozi wa Old Trafford.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna tangazo rasmi la Manchester United kuhusu uteuzi wa Pochettino.