Mashabiki Afrika Wasubiri Burudani Mpya: CANAL+ Yapata Haki za UEFA Hadi 2031

CANAL+ imetangaza kupata haki miliki za kuonesha mashindano yote ya klabu za wanaume ya UEFA katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kuanzia katikati ya mwaka 2027, CANAL+ itakuwa ikiwaletea wateja wake mechi kubwa za UEFA Champions League, UEFA Europa League, na UEFA Conference League katika nchi zaidi ya 40 za ukanda huu hadi mwaka 2031.

Mashabiki watafurahia mechi kali zaidi za soka la Ulaya zikizikutanisha klabu bora kutoka England, Ufaransa, Hispania, Italia, Ujerumani na Ureno, pamoja na nyota maarufu kama Victor Osimhen, Ademola Lookman, Serhou Guirassy, Amad Diallo, Bryan Mbeumo, Antoine Semenyo, Nicolas Jackson, Kylian Mbappé, Ousmane Dembélé, Lamine Yamal, Erling Haaland, Michael Olise, Achraf Hakimi, Harry Kane na wengine wengi. Wachezaji hawa wote watakuwa wakionekana kupitia vituo vya CANAL+.

Katika nchi zinazozungumza Kiingereza na Kireno barani Afrika, SuperSport, ambayo kwa muda mrefu imekuwa mtangazaji wa mashindano ya UEFA, itaendelea kuimarisha nafasi yake kama jukwaa linaloongoza kwa matangazo ya michezo na itaendelea kuwaoneshea wateja wake mashindano ya klabu za UEFA kwa haki za kipekee.

Kwa Afrika inayozungumza Kifaransa, makubaliano haya mapya yanaashiria kurejea kwa matangazo kamili ya UEFA Champions League kupitia vituo vya CANAL+ Sport, na kwa mara ya kwanza kabisa, pia kuonesha UEFA Europa League na UEFA Conference League kwa haki za kipekee katika lugha ya Kifaransa, jambo litakalowafurahisha sana wateja wetu.

Vituo vya SuperSport na CANAL+ Sport, ambavyo vina umaarufu mkubwa katika ukanda huu, tayari vinatoa ratiba bora ya soka ikiwemo Betway Premiership, Premier League, LALIGA EA SPORTS, Ligue 1, pamoja na TotalEnergies Women’s Africa Cup of Nations Morocco 2026, ambayo ilianza siku chache zilizopita.

Kupitia ushirikiano huu muhimu na UC3, CANAL+ inaendelea kuimarisha nafasi yake kama makazi ya michezo ya kiwango cha kimataifa, kwa kuwapa wateja wake fursa ya kufurahia mashindano bora zaidi duniani.

“Tunajivunia sana ushirikiano huu mpya ambao umetupatia haki za kipekee za kuonesha mashindano yote ya klabu za wanaume ya UEFA katika zaidi ya nchi 40 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara amesema Maxime Saada, Mkurugenzi Mtendaji wa CANAL+.

Kwa misimu minne ijayo hadi mwaka 2031, wateja wetu watafurahia msisimko wa mechi kubwa za UEFA Champions League, UEFA Europa League na UEFA Conference League. Leo, CANAL+ inatoa mkusanyiko bora zaidi wa maudhui ya michezo katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na upatikanaji wa haki hizi ni ushahidi mwingine wa dhamira yetu hiyo.”

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa UC3 pamoja na timu za Relevent kwa kuendelea kutuamini, kufuatia makubaliano yetu ya hivi karibuni nchini Ufaransa, Uswisi, Ubelgiji, Poland na Austria.” Alisisitiza Maxime.