HOUSTON, Marekani – Nahodha msaidizi wa Brazil, Marquinhos, amesema timu yake imeimarika kwa kiwango kikubwa na iko tayari kuikabili Japan katika mchezo wa hatua ya mtoano wa Kombe la Dunia utakaopigwa Jumatatu.
Brazil inashuka dimbani leo Saa mbili Usiku Juni 29, 2026 ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao 3-2 dhidi ya Japan katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Oktoba mwaka jana, ushindi ambao ulikuwa wa kwanza kwa Japan dhidi ya Brazil katika historia yao.
Hata hivyo, Marquinhos amesema kipigo hicho kiliwasaidia kujifunza na kuboresha makosa yao.
“Kila tulichopitia katika miaka ya hivi karibuni kimetufikisha hapa tulipo sasa. Tulijifunza mengi kutokana na mechi ile na tangu wakati huo tumebadilika na kukua kama timu,” alisema beki huyo wa Paris Saint-Germain.
Aliendelea kueleza kuwa ujio wa kocha Carlo Ancelotti umeleta utulivu, mbinu bora na kuifanya Brazil kuwa timu yenye mshikamano mkubwa.
Brazil ilianza Kombe la Dunia kwa sare ya 1-1 dhidi ya Morocco kabla ya kuifunga Haiti na Scotland mabao 3-0 kila mmoja, na sasa inawania tiketi ya hatua ya 16 bora.
Kwa upande wake, Ancelotti amesema mechi za hatua ya mtoano zinahitaji utulivu wa akili, moyo wa kupambana na umakini mkubwa.
“Timu iko tayari, wachezaji wana morali na wanajiamini. Lakini tunaiheshimu Japan, ambayo ni moja ya timu bora duniani kwa sasa,” alisema kocha huyo raia wa Italia.
Ancelotti pia amesema bado hakuna timu iliyojitokeza wazi kuwa ndiyo favorit wa kutwaa Kombe la Dunia, licha ya mabingwa watetezi Argentina na Ufaransa kuonyesha kiwango kizuri katika hatua ya makundi.