Mbappé Aweka Makazi Kwenye Mtaa wa Mastaa wa Soka

Kylian Mbappé ameanza maisha mapya ya kifahari nchini Hispania baada ya kuhamia kwenye jiji la Madrid kufuatia kujiunga na Real Madrid. Nyota huyo wa Ufaransa anaishi kwenye eneo maarufu la matajiri linaloitwa La Finca, ambalo linajulikana kwa kuwa makazi ya mastaa wa soka, wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu duniani.

Eneo hilo lina ulinzi wa hali ya juu ukiwemo mfumo wa kamera, walinzi wa kudumu pamoja na mageti maalum yanayodhibitiwa kwa usalama mkubwa, jambo linalowapa wakaazi faragha ya kutosha mbali na usumbufu wa mashabiki au paparazi.

Mbappé anaripotiwa kuinunua villa hiyo ya kifahari kwa takriban euro milioni 11, huku nyumba hiyo ikiwa iliwahi kumilikiwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, Gareth Bale. Jumba hilo lina mandhari ya kisasa na huduma zote za kifahari zinazomfaa mmoja wa wachezaji wakubwa duniani kwa sasa.

Ndani ya nyumba hiyo kuna mabwawa ya kuogelea ya ndani na nje, chumba maalum cha sinema, gym ya kisasa pamoja na vyumba kadhaa vya kulala vinavyokadiriwa kufikia saba hadi nane. Pia nyumba hiyo imezungukwa na bustani kubwa yenye ukubwa wa karibu mita za mraba 3,000 inayoongeza uzuri na faragha zaidi.

Kwa kifupi, Mbappé haishi kwenye nyumba ya kawaida ya kukodi bali kwenye moja ya majumba ya kifahari zaidi ndani ya “celebrity zone” ya Madrid, eneo ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa mastaa wengi wa soka duniani.