De Zerbi Afunguka Mpango wa Kuibadili Spurs Baada ya Kunusurika Kushuka Daraja

Roberto De Zerbi, Head Coach of Tottenham Hotspur

Kocha wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi amesema tayari ana maono ya wazi kuhusu nini kifanyike kuirejesha timu hiyo kwenye ushindani mkubwa, lakini mazungumzo hayo yataanza rasmi baada ya mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Everton siku ya Jumapili.

Spurs kwa sasa wanashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Premier League wakiwa na tofauti ya pointi mbili juu ya West Ham United huku wakibebwa na faida ya mabao.

Akizungumza na Sky Sports, De Zerbi alisema kila mmoja ndani ya klabu anapaswa kuongeza juhudi ili kuhakikisha timu hiyo inabaki salama kwenye ligi hiyo.

“Nina maono ya wazi kuhusu kile tunachopaswa kufanya, lakini kwanza tunahitaji kuhakikisha tunabaki Premier League. Baada ya saa moja usiku Jumapili ndipo tutakaa kupanga mambo ya msimu ujao,” alisema De Zerbi.

Kocha huyo alikiri kuwa amepitia kipindi kigumu tangu ajiunge na Spurs kutokana na kukuta changamoto nyingi ambazo hakuzifahamu kabla, lakini amejivunia namna alivyojenga mahusiano mazuri na wachezaji, viongozi pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

“Mashabiki hawastahili kuona timu yao ikiwa katika nafasi hii kwenye msimamo,” aliongeza.

De Zerbi pia alisema hafikirii matokeo ya timu nyingine bali anaamini Spurs wanapaswa kupambana wao wenyewe uwanjani ili kupata ushindi muhimu dhidi ya Everton na kujihakikishia kubaki ligi kuu England.