Blues Wazama Baharini! Chelsea Yapigwa Mechi 5 Mfululizo Bila Bao

Klabu ya Chelsea FC imejikuta katika kipindi kigumu baada ya kupoteza mechi tano mfululizo za Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1993, huku pia ikishindwa kufunga bao katika mfululizo huo wa mechi hali ambayo haijawahi kutokea katika kipindi cha miaka 114.

Matokeo hayo yamekuja baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brighton & Hove Albion FC katika dimba la Amex, matokeo ambayo yamezidi kufifisha matumaini ya Chelsea kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Brighton walionyesha ubora wao mapema katika mchezo huo, wakitangulia kupitia bao la dakika ya 3 kabla ya kuongeza mengine katika kipindi cha pili na dakika za majeruhi, na kuondoka na ushindi mnono dhidi ya mabingwa hao wa zamani.

Matokeo haya yanaendelea kuongeza presha kwa Chelsea ambao wamekuwa na msimu mgumu, wakishinda mechi moja tu katika michezo tisa ya mwisho kwenye mashindano yote.

Wataalamu wa soka wanasema kiwango cha timu hiyo kimekuwa kikishuka kwa kasi, huku mashabiki wakitaka mabadiliko makubwa ili kurejesha hadhi ya klabu hiyo kwenye ligi.

FT: Brighton 3-0 Chelsea
⚽ 03’ Kadioglu
⚽ 56’ Hinshelwood
⚽ 90+1’ Welbeck