Vigogo wa soka Tanzania, Simba na Yanga usiku wa kuamkia leo Februari 23, 2026 wameendeleza ushindani mkali wa kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi muhimu katika michezo yao ya jana.
Katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Simba walionyesha ubora wao kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons. Wekundu wa Msimbazi walianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 18 kupitia kwa Selemani Mwalimu ‘Gomez’, aliyemalizia vyema shambulizi lililoandaliwa kwa ustadi.
Simba waliendelea kulisakama lango la Prisons na juhudi zao zikazaa matunda tena dakika ya 45+1 baada ya beki Rushine De Reuck kufunga kwa mkwaju wa penalti, kufuatia madhambi ndani ya eneo la hatari. Bao hilo liliwahakikishia Simba kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele, hali iliyodumu hadi filimbi ya mwisho.
Wakati huo huo, katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, Young Africans SC walilazimika kupambana vilivyo kabla ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC. Bao pekee la mchezo lilifungwa dakika ya 26 na mshambuliaji Laurindo Dilson Maria ‘Depu’, aliyemalizia kwa ustadi mpira wa ndani ya boksi na kuwanyamazisha mashabiki wa wenyeji.