Klabu ya Al Ahly SC imetangaza kutoa mabasi ya bure kwa ajili ya kuwasafirisha mashabiki wake kwenda Alexandria, ambako timu hiyo itavaana na Yanga SC siku ya Ijumaa katika mchezo muhimu wa kimataifa.
Awali, mechi hiyo ilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, hata hivyo imehamishiwa kuchezwa katika dimba la Alexandria, hatua iliyowalazimu viongozi wa Al Ahly kuchukua uamuzi wa kuwezesha usafiri wa mashabiki wao ili kuhakikisha timu inapata sapoti kubwa ugenini.
Uwanja wa Alexandria upo umbali wa takribani kilomita 568 kutoka Cairo, jambo lililofanya klabu hiyo kuandaa usafiri maalum kwa mashabiki wake kama sehemu ya motisha na mshikamano kuelekea mchezo huo.
Wakati huo huo, Al Ahly wameendelea na mazoezi makali ya maandalizi, wakipata morali kubwa kufuatia kurejea kwa wachezaji wao waliokuwa kwenye majukumu ya kimataifa, hususan waliokuwa wakishiriki Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Urejeo wa nyota hao unatajwa kuipa Al Ahly nguvu mpya kuelekea pambano hilo linalotarajiwa kuwa gumu, huku Yanga SC nao wakitarajiwa kupambana vikali kusaka matokeo chanya ugenini.
Mechi hiyo inatajwa kuwa moja ya michezo inayosubiriwa kwa hamasa kubwa na mashabiki wa soka barani Afrika, kutokana na historia na ubora wa timu zote mbili.