Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Ndege maalum (Boeing 787-8 Dreamliner) kwenda nchini Morocco kuwafuata wachezaji na kuwarudisha nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amesema Rais Samia ametoa ndege hiyo itakayowasafirisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi walioko nchini humo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Paul Makonda ikiwa ni kutambua heshima kubwa waliyolijengea Stars katika mashindano hayo makubwa Barani Afrika licha ya kuondolewa na wenyeji Morocco katika hatua ya 16 ambayo hawakuwahi kuifikia.
Taarifa ya Msigwa inasema kuwa pamoja na kuwatumia ndege hiyo, Rais Samia ameandaa hafla ya chakula cha mchana itakayofanyika Januari 10, 2026 katika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapongeza rasmi pamoja na wanamichezo wengine.
Ndege hiyo inatarajiwa kuondoka Jijini Dar es Salaam leo tarehe 6 Januari, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri na itawasili Jijini Rabat Morocco leo majira ya saa 4:30 usiku, kisha itaondoka Jijini Rabat Morocco tarehe 7 Januari, 2026 na kuwasili Jijini Dar es Salaam siku hiyo majira ya saa 2:00 usiku katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.