MWAKINYO AVULIWA UBINGWA

HABARI mbaya kwa Watanzania na mashabiki wa ngumi ni kwamba Shirikisho la ngumi za kulipwa duniani limewavua mikanda ya ubingwa wa WBF Intercontinental mabondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ‘Champez’ na Ibrahim Class kutokana na kutotetea mikanda hiyo kwa muda mrefu tofauti na sheria zake.

 Rais wa Shirikisho hilo, Howard Goldberg kutoka Afrika Kusini yalipo makao makuu ya Shirikisho hilo ambapo amekiri kuhusu mabondia hao kuvuliwa ubingwa wa mikanda hiyo kutokana na kukaa nayo muda mrefu bila ya kutetea tofauti na sheria za WBF zilivyo.

“Ni kweli tumewavua ubingwa wa WBF Intercontinental, Hassan Mwakinyo na Ibrahim Class ambao walishinda katika pambano yalioandaliwa na Jackson Group kwa sababu hakuweza kutetea kwa wakati.

“Sasa mikanda ipo wazi katika uzani wa Super Walter Kg 70 na Super Feather Kg 59 kwa sababu sheria walitakiwa kuitetea katika kipindi cha miezi sita lakini mtu kama Mwakinyo aliacha kutetea na kwenda kuwania mkanda mwingine wa Ubingwa wa Afrika (ABU) tena mara mbili,” alisema Goldberg.

Ikumbukwe Mwakinyo ameutetea mkanda huo mara moja baada ya kumpiga Jose Carlos Paz raia wa Argentina huku Class akishinda kwa mara ya kwanza kufuatia kumtwanga Denis Mwale wa Malawi.

Mwakinyo na Class wanaingia kwenye orodha ya mabondia wa Tanzania waliovuliwa mkanda wa WBF Intercontinental baada ya mkongwe Francis Cheka ‘SMG kuvuliwa mwaka 2016 baada ya kushindwa kutetea kwa wakati mkanda wake aliompiga Geard Ajetovic.