Staa wa muziki wa Hip Hop nchini Marekani, Sean “Diddy” Combs, amehukumiwa kifungo cha miezi 50 (sawa na miaka 4 na miezi 2) gerezani baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba.
Combs, ambaye amekuwa akishikiliwa katika gereza la Brooklyn, New York tangu kukamatwa kwake mwezi Septemba 2024, alikutwa na hatia ya kuwasafirisha wapenzi wake wawili wa zamani na kuwalazimisha kushiriki ngono na wanaume waliolipwa kwenye sherehe zake binafsi zilizojulikana kama “Freak Offs.”
Kesi hiyo, iliyochukua zaidi ya miezi miwili, iliendeshwa katika Mahakama ya Manhattan msimu wa kiangazi, ikihusisha ushahidi wa kina kutoka kwa waathirika pamoja na mashahidi wengine.
Katika kutoa hukumu, jaji Arun Subramanian alisisitiza kwamba adhabu hiyo inalenga kuwa mfano wa kuzuia visa vya aina hii, akibainisha kwamba unyonyaji na unyanyasaji wa wanawake hauwezi kuvumiliwa.
Mbali na kifungo hicho, Combs pia ameamriwa kulipa faini na atakuwa chini ya usimamizi maalum kwa muda wa miaka mitano baada ya kumaliza kifungo chake.