Kikosi cha klabu ya Simba Sc kitaondoka Nchini kesho Mei 13, 2025 saa 11:00 Alfajiri kuelekea Morocco kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane utakaopigwa Mei 17, 2025 huko Berkane, Morocco.
Akizungumza leo Mei 12, 2025 kwenye mkutano na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amebainisha kuwa safari hiyo itakuwa ya masaa saba (7) moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Casablanca huku akimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha safari hiyo.
“Kikosi kitaondoka kesho saa 11 alfajiri kwenda Morocco. Itakuwa safari ya masaa 7 saba moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Casablanca. Kwa hili hatuna budi kumshukuru sana, tena kumshukuru tena, tena kumshukuru mara elfu, kumshukuru pakubwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Tanzania. Kwa hili ametutendea kubwa sana.”—Semaji Ahmed Ally.