SIMBA YATOA TAMKO ISHU YA MPANZU KUCHEZA KITAIFA NA KIMATAIFA

AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kumekuwa na maswali mengi kuhusu lini Mpanzu atacheza jambo ambalo limemfanya atolee ufafanuzi suala hilo.

Ikumbukwe kwamba nyota huyo yupo na kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids bado hajacheza mchezo wowote wa ushindani msimu wa 2024/25.

Ally amesema: “Desemba 15 litafunguliwa dirisha dogo la usajili wa ndani na Ellie Mpanzu atasajiliwa hapo kwa maana hiyo mechi yoyote ya ndani baada ya tarehe 15 atakuwa sehemu ya kikosi lakini dirisha la CAF ni mpaka Januari, 2025 kwahiyo mechi yoyote ya kimataifa kuanzia Januari atakuwa sehemu ya kikosi.

“Hivyo kwa mechi zote za ligi kuanzia Desemba 15 Mpanzu atacheza kwa kuwa usajili utakuwa umefunguliwa lakini kwenye mechi za kimataifa usajili wake ni mpaka Januari, hivyo yeye katika mechi za kimataifa ataanza kucheza Januari na hata hivyo Januari sio mbali ujue.”

Simba ipo kwenye hesabu kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien, Desemba 15 Uwanja wa Mkapa hivyo Mpanzu hatakuwa sehemu ya kikosi.

Kwa mechi za Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC, Simba imekuwa ikitumia Uwanja wa KMC kwa mechi za nyumbani ambao kwa sasa pia hata Yanga watakuwa wakiutumia baada ya kuhama Azam Complex.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.