IMEBAINIKA kuwa mabosi wa Simba wapo katika harakati za kumrudisha kiungo mkabaji Gerson Fraga raia wa
Brazil kwa ajili ya kuziba pengo la kiungo Taddeo Lwanga ambaye amekuwa na majeraha ya mara kwa mara Lwanga ameshindwa kuitumikia Simba katika ligi kuu mara baada ya kuumia katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Jwaneng Galaxy ambapo katika mchezo huo Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-1.
Simba kwa sasa wamekuwa wakiwatumia viungo Jonas Mkude, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin katika eneo
hilo la kiungo wa chini lakini inaelezwa kuwa benchi la ufundi halijaridhishwa na viwango vya wachezaji hao katika idara ya ukabaji.
Chanzo cha ndani kutoka Simba kimeliambia Championi Jumamosi kuwa uongozi wa timu hiyo upo katika harakati za kufanya usajili wa kiungo mmoja wapo mkabaji huku tayari wakiwa wameshafanya mazungumzo na Fraga na
Shiboub baada ya kubainika kuwa ana tatizo kubwa kwenye goti lake.
“Simba ipo katika mazungumzo na baadhi ya wachezaji wakiwemo Fraga na Shiboub kwa ajili ya kuja
kuziba pengo la Lwanga ambaye mpaka sasa kuna asilimia kubwa huenda nyota huyo akatemwa kutokana na kuwa na majeraha ya goti.
“Lwanga ana tatizo kubwa ambalo linahitaji upasuaji utakaomuweka nje kwa muda mrefu jambo ambalo timu itahitaji kupata mbadala wake kwa kuwa inakabiliwa na mashindano makubwa ya kimataifa na kuhitaji kuutetea ubingwa wa ligi kuu msimu huu hivyo usishangae kama Lwanga ataachwa na Simba,” kiliweka wazi chanzo hicho.
Championi Jumamosi, lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Maudhui ndani ya Simba, Ally Sharty, kwa aajili ya kuweka wazi ishu hiyo ambapo alisema: “Kuhusu Lwanga kuachwa na Simba ni tetesi tu wala hakuna mpango wa kumuacha.
“Bado ana mkataba halali wa kuendelea kuitumikia Simba, ni kweli Lwanga anasumbuliwa na majeraha lakini kwa sasa yupo vizuri na akishakuwa fiti basi ataonekana uwanjani,” alisema kiongozi huyo.