NYOTA wa Tabora United, Najim Musa ameweka wazi kuwa sababu kubwa iliyowafanya wakapoteza mchezo wao dhidi ya Simba, Uwanja wa Azam Complex ni kutokuwa na bahati.
Kwenye mchezo uliochezwa Mei 6 2024 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Simba 2-0 Tabora United pointi tatu zikibaki kwa Mnyama, Simba.
Ikumbukwe kwamba Musa kwenye mchezo huo alikuwa kwenye ubora dakika ya 76 alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 lilimshinda mlinda mlango Ayoub Lakred na lilikuwa linaonekana kama limevuka mstari.
Kutokana na pigo hilo wachezaji wa Tabora United walionekana kumzonga mwamuzi wa kati Amina Kyando ili awape bao lakini walichelewa kwa kuwa Simba walifanya shambulizi la kushtukiza likawapa bao dakika ya 77 kupitia kwa Edwin Balua.
Musa amesema; “Haikuwa bahati yetu nadhani kwa kuwa tulipambana kupata matokeo tukashindwa kupata wapinzani wetu wakapata ushindi.
“Kwa upande wa bao nadhani mwamuzi wa pembeni alikuwa na nafasi nzuri yakuamua kama ilikuwa ni bao ama la, ni makosa ya kibinadamu haya. Wakati tukiwa tumemfuata mwamuzi tulipoteza concetration, hivyo wao wakafanya shambulizi lakushtukiza wakapata bao,”.