ALIYEWAMALIZA SIMBA KIMATAIFA YUPO TAYARI KUVAA UZI MWEKUNDU

MSHAMBULIAJI Mnamibia wa timu ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, Rudath Wendell ambaye alifunga mabao mawili dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Mkapa, katika mchezo wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika ameweka wazi kuwa yupo tayari kujiunga na Yanga ikiwa watapeleka ofa inayoeleweka.

Oktoba 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Wendell mwenye umri wa miaka 26 alifanikiwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata Galaxy na kuwaondosha Simba katika mashindano hayo kwa faida ya bao la ugenini.

Katika mchezo huo, Wendel aliingia kipindi cha pili na kufunga mabao hayo dakika ya 46 na 59 ya mchezo.

Wendell alisema: “Ni kweli kuna baadhi ya viongozi wa timu za Tanzania walionyesha kuvutiwa na kiwango ambacho nilionyesha kwenye mchezo dhidi ya Simba huko Tanzania, lakini hakuna mazungumzo rasmi ambayo tumeyafanya.

“Kwa sasa mimi bado ni mchezaji wa Galaxy kutokana na mkataba nilionao, lakini mkataba huo una kipengele kinachoweza kuniruhusu kuondoka ikiwa kuna timu itafikia makubaliano ya kuvunja mkataba na ni matamanio yangu kuona siku moja nacheza soka kwenye timu kubwa huko Tanzania, Simba au hata wapinzani wao.

“Mimi nipo tayari kama Simba wakija hata kesho kila kitu kikaa tayari nakwenda kucheza soka kwa kuwa hii ndiyo ajira yangu.”