MADAKTARI wa Yanga wanaangalia uwezekano mkubwa wa kumpa kifaa maalum cha ‘Mask’ kiungo wake mpya Augustine Okrah aliyepata jeraha eneo la puani.
Kiungo huyo alipata majeraha hayo katika Kombe la Mapinduzi mwezi Januari, baada ya kugongana na mchezaji wa timu pinzani na kupata majeraha katika mishipa ya puani.
Nyota huyo aliyejiunga na Yanga katika dirisha hili dogo yupo nje ya uwanja akiendelea kuuguza majeraha hayo aliyoyapata.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa kiungo huyo anaendelea na matibabu huku akiwa chini ya uangalizi wa madaktari ili kuhakikisha anarejea mapema uwanjani kuipambania timu yake.
Kamwe alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kurejea akiwa katika muonekano tofauti wa kuvaa ‘Mask’ kama ambayo anayovaa mshambuliaji raia wa Nigeria, Victor Osimhen anayeichezea Klabu ya Napoli ya nchini Italia.
“Okrah anaendelea vizuri hivi sasa, yupo katika matibabu maalum yatakayomrejesha mapema uwanjani katika michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa.
“Kutokana na aina ya jeraha ambalo amelipata sehemu ya usoni, upo uwezekano mkubwa kuvaa Mask usoni mwake kwa ajili ya kujilinda zaidi kama anavyovaa Osimhen,” alisema Kamwe.