NYOTA Reliants Lusajo ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram wa kuiaga familia yake ya Namungo alikokuwa akipambania majukumu yake.
Namungo inashiriki Ligi Kuu Bara inatumia Uwanja wa Majaliwa kwa mechi za nyumbani.
Dirisha dogo la usajili tayari limefunguliwa tangu Desemba 16 na wachezaji wanatoka na kuingia kwenye klabu tofauti ambapo ameweka wazi kwamba anakwenda kupata changamoto sehemu nyingine.
Geita Gold na Tabora United zinatajwa kuwa kwenye hesabu za kuiwinda saini ya nyota huyo ambaye ni mshambuliaji.
Katika ujumbe wake huo, Lusajo ameandika; “Napenda Kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Namungo na benchi la ufundi bila kusahau mashabiki wote wa timu ya Namungo kwa kipindi chote tulichokuwa pamoja. Ni muda wangu sasa wa kuangalia changamoto sehemu nyingine. Nipende kuwatakia kila la kheri katika msimu huu wa ligi.”
Ikumbukwe kwamba nyota huyo alirejea kwa mara nyingine ndani ya Namungo 2021 akitokea Klabu ya KMC.