NYAKATI ngumu hazidumu lakini zina maumivu makubwa kwa anayekutana nazo hivyo ni muhimu kutafuta njia nzuri ya kuepukana na hayo kwa umakini, hivyo tu basi.
Wawakilishi wa Tanzania kwenye anga la kimataifa, Simba wanapita kwenye nyakati za maumivu kwa wachezaji kushindwa kupata ushindi katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika zaidi ya kuambulia sare.
Ikumbukwe kwamba walianza na Power Dynamos 2-2 Simba na ule mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ilikuwa Simba 1-1 Power Dynamos.
Kivumbi kilianza kwenye hatua za makundi kete ya kwanza, ubao wa Uwanja wa Mkapa, Novemba 25 ulisoma Simba 1-1 ASEC Mimosas, Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba anabainisha hali halisi namna hii:-
“Kwenye mechi za kimataifa ambazo ni kutafuta nafasi ya kufika robo fainali mechi za nyumbani ni muhimu kupata pointi tatu.
“Unatakiwa kushinda ili kutengeneza hali ya kujiamini kwa wachezaji na kwa ajili ya kupata matokeo mechi zinazofuata. Kuanza kwa kupoteza pointi mbili haya ni matokeo yanayoleta picha kwamba tunakazi ngumu ambayo tumejiongezea kufanya hapo baadaye.
Mwendo wa mechi za kimataifa upoje?
“Huu ni mwendelezo wa makosa ambayo tumekuwa nayo kwenye mechi zilizopita kitaifa na kimataifa.Hivyo ni muhimu kurejea kwa mara nyingine tukiwa imara na kupata kile kilicho bora. Hayakuwa matokeo ambayo tulikuwa tunahitaji lakini yameshatokea.
“Kwenye mechi za kimataifa ambazo sita ni lazima ushinde zote tatu za nyumbani ukishapoteza mechi moja ama kupata sare maana yake kwenye mechi tatu za ugenini ni lazima ushinde mechi moja ya ugenini kufikisha zaidi ya pointi tisa.
“Mwaka jana iliwezekana, tulipoteza dhidi ya Raja Casablanca lakini tukamfunga Horoya nje ndani. Sasa maisha huwa yanabadilika inawezekana mwaka huu tusipate wa kumfunga nyumbani kwake.
“Lakini tuna kazi ya kufanya kuhakikisha kwamba tunatafuta ushindi kwenye mechi moja ugenini na zilizobaki nyumbani mbili zote tunapaswa kupambana ili kupata ushindi.
Mashabiki kutojitokeza kwa wingi uwanjani hili lipoje?
“Hapo hakuna kingine ambacho tunapaswa kusema kwa sasa zaidi ya kutafuta matokeo. Mashabiki wanapenda furaha na furaha inapatikana kwenye matokeo.
“Wapo mashabiki wa aina tofauti wapo wale ambao muda wote wapo na timu na wengine wanafurahia kuona timu ikiwa inacheza vizuri. Tukianza kupata matokeo mazuri mashabiki watajitokeza kwa wingi na hilo halijifichi matokeo ni muhimu.
“Wachezaji wanatambua hilo, benchi la ufundi linatambua hilo hivyo kwa mechi zinazofuata tunaamni kwamba tutapata matokeo mazuri.
Mchezo ujao ugenini hesabu zipoje?
“Tunakwenda kucheza na Jwaneng Galaxy hawa ni wapinzani wazuri na watatupa ushindani. Ambacho tunakwenda kufanya ni kutafuta ushindi kufikia malengo ambayo tumejiwekea.
“Furaha kubwa inabebwa na matokeo hivyo makosa yaleyale kwenye mechi zilizopita yanapaswa kufanyiwa kazi kuwa na mwendelezo mzuri. Hizi ni nyakati ngumu ambazo tunapita na hakuna ambaye anaweza kututoa hapa tulipo.Sisi wenyewe tunapaswa kujitoa hapa na kuwa kwenye mwendo bora.
“Malengo yapo na tunaamini kila kitu kitakuwa sawa lakini sio maneno mengi kwa sasa bali inahitajika vitendo zaidi kwenye mechi zetu za kitaifa na kimataifa. Tunawafuata wapinzani wetu Jwaneng Galaxy tukiwa na tahadhari na tukitambua kwamba ushindani Ligi ya Mabingwa ni mkubwa.
“Tunahitaji kufika robo fainali kwenye mashindano haya makubwa lakini haitakuwa rahisi ni lazima tupambane. Mashabiki tuzidi kushikamana kwenye nyakati hizi ngumu ambazo tunapitia tunazidi kuimarika,” anamaliza Ally.
Makala haya yameandikwa na Dizo Click na kutoka gazeti la Spoti Xtra.