>

YANGA YAANZA KWA KUPOTEZA UGENINI

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa Yanga kete yao ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika wameanza kwa kupoteza mchezo huo.

Ni usiku wa kuamkia leo Novemba 25 Yanga ilitupa kete yake ya kwanza ugenini kusaka pointi tatu dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ilikuwa imara kwenye umiliki wa mpira na pasi nyingi lakini wapinzani wao walicheza kwa mbinu ya kusaka ushindi.

Baada ya dakika 90 ubao ulisoma CR Belouizdad 3-0 Yanga na langoni alianza kipa namba mbili Metacha Mnata huku ukuta ukiwa na Dickson Job, Bacca waliokuwa na kazi ya kuzuia hatari za wapinzani wao.

Mabao ya Benguit dakika ya 10, Bantahar dakika ya 45 na lile la tatu lilijazwa kimiani na Jallow dakika ya 90.

Baada ya mchezo huo Yanga inarejea Bongo ambapo kete yake inayofuata ni dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Desemba 2 2023.