>

MANULA KUIKOSA ASEC MIMOSAS CHAMA HATIHATI

WAKIWA kwenye maandalizi ya mwisho kuwakabili wapinzani wao ASEC Mimosas kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba watakosa huduma ya nyota wao wawili.

Kwa mujibu wa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Daniel Cadena ameweka wazi kuwa maandalizi yapo vizuri isipokuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kukosekana kwenye mchezo huo.

Ni Uwanja wa Mkapa, Novemba 25 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa ambapo Simba watakuwa wenyeji dhidi ya ASEC Mimosas.

Kocha huyo amesema: “Huenda kwenye mchezo wa kesho tukawakosa baadhi ya wachezaji wetu ambao ni Aishi Manula mwenye maumivu chini ya mguu wake na Clatous Chama.

“Chama yeye amewasili jana akitokea Zambia, tutaona kama itawezekana kumtumia dhidi ya Asec Mimosas. Maandalizi yapo vizuri na tunatambua kwamba utakuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa.

“Wachezaji wapo tayari na wanatambua kwamba mashabiki wanapenda kuona tukipata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu,” amesema.