KAZI BADO IPO KWENYE LIGI, MAKOSA YAFANYIWE KAZI

MZUNGUKO wa kwanza una ushindani mkubwa na kila timu kuwa kazini kusaka pointi tatu. Mechi za mwanzo zinatoa picha ya kile ambacho kipo ndani ya timu husika.

Kila idara ni muhimu kuwa imara ili kupata matokeo chanya. Kuanzia safu ya ulinzi na ushambuliaji hapa kuna ulazima wa kutazama mapungufu ambapo yalionekana kwa mechi zilizopita.

Ikiwa timu ilitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia, benchi la ufundi lina kazi kuboresha katika eneo la ushambuliaji. Ili upate ushindi kwenye mechi za ligi ni lazima ufunge.

Kama washambuliaji watakwama kufunga ina maanisha kwamba kupata ushindi kwenye mechi zijazo pia itakuwa ni mtihani. Kwa wachezaji nao wanaona namna ushindani ulivyo hivyo nao watachukua hatua.

Upande wa ulinzi ni muhimu nao kuangalia idadi ya mabao ambayo waliruhusu kwenye mechi zilizopita. Kuna umuhimu wa kila idara kuwa bora kutengeneza muunganiko mzuri.

Mabao yanayopatikana kupitia safu ya ushambuliaji ni muhimu kulindwa ili kupata huo ushindi. Dakika 90 za kusaka pointi tatu jasho kila kona linavuja kuanzia ushambuliaji mpaka ulinzi.

Kwa timu ambazo hazikuwa na mwendo mzuri kwenye mechi za mwanzo muda uliopo ni sasa kufanyia maboresho makosa yaliyopo kwa ajili ya kupata matokeo kesho.

Kila kitu kinawezekana ikiwa makosa yatafanyiwa kazi na wale waliokosea wakakubali kufundishika. Benchi la ufundi hakuna muda mwingine wa kufanyia kazi makosa ni sasa.