ISHU YA JOB KUROGWA YANGA IPO HIVI

KATI ya mkoa ambao umebarikiwa vipaji vya soka basi ni Morogoro uliozalisha vipaji vingi katika Ligi Kuu Bara
ndani ya misimu mitano mfululizo.

Kati ya wachezaji waliozalishwa na kuwa gumzo kwa misimu ya karibuni ni Kibwana Shomari, Dickson Job, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Hassani Kessy, Aishi Manula na wengine wengi.

Kati ya hao, wachezaji ambao hivi sasa wanatajwa kuwa katika viwango vikubwa, jina la Job halikosekani ambaye ameonekana kuwa gumzo, kutokana na uimara na kuwa tegemeo katika kikosi cha Yanga.

Wakati anatua Yanga, hakuanza kucheza moja kwa moja, alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hali iliyomfanya kukaa nje kwa muda mrefu.

Spoti Xtra, limefanya mazungumzo maalum na baba wa beki huyo, Nickson Job na kikubwa akizungumzia safari ya maisha ya mwanaye mara baada ya kusajiliwa na Yanga.

UNAZUNGUMZIAJE KIWANGO CHA MWANAO HIVI SASA?
“Mimi sina hofu kabisa na mwangu juu ya kiwango chake ndani ya uwanja, kikubwa anajielewa na anafahamu nini cha kufanya uwanjani.

“Ninaweza kusema kuwa Job amerithi kwa babu yake ambaye ni baba yangu mimi, hapendi masihara licha ya upole aliokuwa nao.

“Upole wake unakuwa ni nje ya uwanja, lakini ndani ya uwanja sio mpole kabisa, nafurahia kuwa na mtoto
wa aina hiyo ambaye katika kazi yake yupo makini.

“Nakumbuka babu yake ambaye mimi baba yangu alikuwa hataki masihara kabisa, ninafikiri yeye karithi kutoka kwake.

 

JOB AMERITHI KIPAJI KWA NANI?
“Sisi familia yetu ni ya soka tangu muda mrefu, mimi nilicheza soka la kiwango cha kawaida cha mitaani tofauti na mwanangu inawezekana kwake kutokana
na ubora na kiwango kikubwa alichonacho hivi sasa.

KIPI KILIWAHI KUMKUTA JOB AKIWA YANGA?
“Nisingependa kuzungumzia hilo, lakini kikubwa ni hali ya ushirikina ambayo inawapata wachezaji wengi wakiwa wanazichezea klabu kubwa kama hiyo ya Yanga.

“Akiwa anajiunga na Yanga, nakumbuka alikaa nje ya uwanja muda mrefu bila ya kucheza baada ya kupata majeraha ya goti.

“Kiukweli nilijaribu kuzungumza naye nini kimempata na kusababishia yeye kukaa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na majeraha yake.

“Katika mazungumzo yangu alinielezea kukutana na masuala ya kishirikina ya yeye kurogwa mara bada ya kujiunga na Yanga.

“Kama baba sikupenda kumshauri chochote kuhusiana na hilo, zaidi nilimtaka kuachana na masuala hayo ya kishirikina na badala yake kucheza soka.

“Kikubwa sikutaka kuweka mbele na kuyaamini masuala ya kishirikina na kumtaka kumuamini Mungu kwa kumuomba ili kufanikisha malengo yake katika soka.

“Kama ningetaka kuyaamini masuala hayo ya kishirikina na kumshauri vibaya, basi ningeharibu malengo na ndoto zake.

“Nashukuru nilifanikiwa katika hilo na kumtaka kucheza soka na kuweka pembeni masuaala ya kishirikiana kwa kumtaka asiyaamini kabisa.

“Jambo la kushukuru yeye alitulia na kupata matibabu hospitalini na kumuomba Mun-gu, leo hii amepona na kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na tegemeo.

“Nimshauri kuachana na hayo mambo ya kishirikina, yeye kikubwa aelekeze nguvu na akili zake katika soka pekee hiyo ndiyo silaha yake.

JOB STAREHE YAKE NI IPI?
“Najivunia kuwa na mtoto wa aina tofuti kabisa, Job yeye starehe yake kubwa ni kucheza soka pekee, hicho ni cha kumpongeza.

“Ni tofauti kabisa na mimi ambaye ninavuta sigara na kunywa pombe, yeye hatumii starehe yoyote zaidi ya soka, hivyo nafurahia kuwa na mtoto wa aina hiyo.

“Ninaamini kama akiendelea hivyo, basi atafika mbali katika mafanikio ya soka ikiwa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, nimtakie kila la kheri mwanangu,” anasema Nickson ambaye ni baba mzazi wa Dickosn Job

Job alijiunga na Yanga kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar.