WAAMUZI HAWA MAAMUZI YAO NI PASUA KICHWA

WAAMUZI wengi Bongo wamekuwa pasua kichwa hasa pale wanapopewa jukumu la kusimamia sheria 17 kwenye mechi zinazowahusu Simba na Yanga kutokana na rekodi zao kuwa na utata.

Asilimia kubwa waamuzi hao wameonekana kushindwa kwenda na kasi ya mchezo ama kufanya vizuri mwanzo ila ikifika mwisho wanaboronga mazima kwa mujibu wa rekodi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, (TBLB), Steven Mguto alisema kuwa kuhusiana na changamoto za waamuzi hii imekuwa ni hoja ambayo inajirudia mara kwa mara si kwenye ligi yetu bali hata kwenye ligi za nje.

Hii hapa ni orodha ya baadhi ya waamuzi wa mechi ambazo zilichezwa kwa msimu wa 2021/22 zilizowahusu Simba na Yanga namna walivyokuwa ni pasua kichwa kwa upande wa maamuzi yao ambayo yalileta utata:-

Hance Mabena, huyu alichezesha mchezo wa Mbeya Kwanza 0-2 Yanga uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Katika mchezo huu alikuwa kwenye mwendo mzuri mwanzo mwisho ila alikuja kuboroga alipowanyima Mbeya Kwanza penalti baada ya kuonekana Bakari Mwamnyeto akimchezea faulo mchezaji wa Mbeya Kwanza ndani ya 18 ilikuwa ni Novemba 30.

Abel William kipimo chake ilikuwa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Ilulu na ulikamilika kwa ubao kusoma Namungo 1-1 Yanga ilikuwa ni Novemba 20.Katika mchezo huu alibebeswa zigo la lawama kwa kutoa penalti ambayo ilionekana na utata baada ya kile alichoona kuwa Feisal Salum alichezewa faulo ndani ya 18 na bao likafungwa na Said Ntibanzokiza.

Pia William mwamuzi huyu alikuwa mwamuzi kwenye mchezo wa ligi kati ya Simba 1-0 Polisi Tanzania,Oktoba 27 Uwanja wa Mkapa ambapo alilalamikiwa kwa kitendo cha kutoa penalti kwa Simba baada ya Bernard Morrison kuonekana akichezewa faulo ndani ya 18 jambo ambalo wachezaji walionekana wakimlalamikia.

Emmanuel Mwandembwa, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa,Novemba 2, na ubao ukasoma Yanga 3-1 Ruvu Shooting, Mwandembwa aiingia kwenye lawama baada ya kutoa penalti kwa Yanga huku mchezaji ambaye alishika mpira ikidaiwa kwamba alikuwa ni mali ya Yanga.

Penalti hiyo ilifungwa na Djuma Shaban jambo ambalo liliwafanya wachezaji wa Ruvu Shooting kutokuwa na furaha na mchezaji wao aliyemchezea faulo Fiston Mayele alionyeshwa kadi ya njano alikuwa Ally Mtoni, ‘Sonso’.

Martin Saanya, huyu amekuwa gumzo kwa sasa baada ya kulifuta bao la George Mpole wa Geita Gold kwa kile kilichotafsiriwa kwamba mfungaji kabla ya kumtungua Aishi Manula alimchezea faulo Shomari Kapombe.

Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Simba 2-1 Geita Gold jambo ambalo limezidi kuwa pasua kichwa kwa wanaochezesha mechi za Simba na Yanga.