MTAMBO HUU WA MABAO YANGA KUWAKOSA WAARABU

IMELEEZWA kuwa mshambuliaji wa Yanga, Hafidh Konkoni huenda akaukosa mchezo wa marudiano wa Hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakaocheza dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.

Mchezo unatarajiwa kupigwa Septemba 30, mwaka huu saa moja kamili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Straika huyo hivi sasa anapambania nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, kinachonolewa na Muargentina Miguel Gamondi.

Taarifa kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyoya Yanga, zilieleza kuwa mshambuliaji ataukosa mchezo kutokana na majeraha ya misuli.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mshambuliaji huyo alipata majeraha akiwa mazoezini kambini kwao Kijiji cha Avic Town, Kigamboni Dar na hivi sasa anaendelea na matibabu.

Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo atarejea uwanjani haraka baada ya majibu ya madaktari kutoa taarifa za kutopata majeraha makubwa yatakayomsababishia kuukosa mchezo huo.

“Konkoni amepata majeraha akiwa mazoezini katika kambini Avic Town, Kigamboni lakini majeraha yatamfanya akae nje kwa siku chache kwa hofu kujitonesha.

“Taarifa za awali zinaeleza kwamba upo uwezekano jeraha hilo likamweka nje kwa muda wa wiki tatu hadi nne ili aweze kurejea katika hali ya kawaida hivyo ataukosa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ali Kamwe kuzungumzia hilo simu yake iliita bila ya mafanikio ya kupokelewa.