BETO YA VIUNGO SIMBA NI PASUA KICHWA

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto
Oliveira amefichua mpaka sasa
hana presha yoyote juu ya safu yake ya kiungo
kutokana na ubora mkubwa unaonyeshwa na
viungo wake wa kati, Mzamiru Yassin na
Fabrice Ngoma hali inayopelekea kupata
ugumu wa chaguo la kwanza.

Ikumbukwe kwamba Simba ilipishana na taji la ligi msimu wa 2022/23 liliobukia Jangwani pamoja na Ngao ya Jamii pia ilikwenda Yanga.

Msimu wa 2023/24 ni Yanga wamekuwa mashuhuda wa Simba wakitwaa Ngao ya Jamii kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Robertinho ametoa kauli hiyo kutokana na
ubora wa viungo hao katika eneo la kati kwa
kuweza kuituliza timu na kuweza kutengeneza
mashambulizi ambapo mpaka sasa Simba
imefanikiwa kushinda mechi nne za
mashindano zikiwemo mbili za Ligi Kuu Bara.

Robertinho amesema kuwa ubora mkubwa
unaonyeshwa na safu yake ya kiungo cha kati
kinapelekea kutokuwa na mchezaji mwenye
nafasi ya uhakika kutokana na wote kuwa
kwenye ubora unaofanana katika kutekeleza
majukumu ya timu ndani ya uwanja.

“Timu ipo kwenye wakati mzuri kwa ajili ya
mashindano ambayo yapo mbele yetu
kutokana ukubwa wake, ukiangalia tuna Ligi ya
Mabingwa Afrika, Super League, Kombe la FA
pamoja na michuano ya Mapinduzi.

“Lakini napata furaha zaidi kwa sababu karibu kila idara wachezaji wamekuwa wakionyesha ubora wa kiwango kikubwa ambacho kinachangia kupata matokeo mazuri.

“Hakuna ambaye anaweza kusema anaweza
kuwa na nafasi ya kudumu ndani ya timu yangu
kwa sababu wote wamekuwa katika ubora
mkubwa, angalia eneo la kati kuna Mzamiru,
Ngoma pamoja na Sadio Kanoute, ambao wote
wanaisadia timu kwa kutimiza majukumu yao
kwa kila ambaye anayepata nafasi ya kucheza,”
amesema Robertinho.