MUHIMU KULINDANA KWA WACHEZAJI HIVYO TU BASI

MUDA mrefu ambao wachezaji wameutumia kwenye maandalizi ya msimu mpya sasa unakwenda kuonyesha matokeo yake uwanjani.

Ni Ngao ya Jamii inatarajiwa kufanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa timu nne kushiriki kuanzia hatua ya nusu fainali ya kwanza ambapo Yanga, Azam FC, Singida Fountain Gate na Simba hizi ni timu shiriki.

Mchezo wa nusu fainali ya kwanza unatarajiwa kuwa kati ya Yanga dhidi ya Azam FC Agosti 9 na ile nusu fainali ya pili inatarajiwa kuwa Agosti 10 Simba v Singida Fountain Gate.

Kila mmoja anatambua kile ambacho alipanda anakwenda kukivuna kweye mechi za ushindani kuanzia mechi za kitaifa na kimataifa.

Pia timu hizi nne zinashiriki mashindano ya kimataifa Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC na Singida Fountain Gate Kombe la Shirikisho Afrika.

Ngoma nzito inakuja kwa wachezaji ambao wamekuwa wakifikiria tofauti na wengine katika kutimiza majukumu yao na mwisho kuwa chanzo cha matatizo kwa wachezaji wengine.

Ipo wazi kwamba kuna wachezaji ambao walishindwa kuwa kwenye ubora wao baada ya kuumizwa makusudi na wachezaji wenzao katika mechi za ushindani.

Hii hapo sawa kwa msimu mpya ni lazima kuwe na utofauti kwa kila mchezaji kulinda usalama wa mchezaji mwenzake.

Itakuwa vizuri kila mchezaji akikamilisha majukumu yake kwa umakini bila kupeleka maumivu kwa mchezaji mwingine.

Furaha ya mashabiki ipo kupata burudani na sio kushuhudia mchezaji anaumia uwanjani tena akiumizwa na mchezaji wa timu pinzani.

Mpira sio uadui ni kazi ambayo inapaswa kufanywa kwa umakini licha ya misuguano ambayo inakuwepo uwanjani kuna faulo ambazo hazina ulazima kwa mchezaji kucheza.

Ikiwa inatokea mchezaji hana mpira na hata mpira akiwa nao hauna hatari kwa timu husika kuna umuhimu gani wa kucheza faulo mbaya ilihali kuna mbinu za kuzuia njia za huo mpira?
Msimu ukawe na ushindani mkubwa huku kila mchezaji akiwa mlinzi wa mchezaji mwingine hivyo tu basi.