UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa masuala yote yanayohusu usajili yapo mikononi mwa benchi la ufundi hivyo wao wakitoa ripoti uongozi unafanya kazi ya kuwaleta wachezaji hao.
Kwa msimu wa 2021/22 mabosi wa Azam FC wameshudia timu hiyo ikiwa kwenye mwendo wa kusuasa baada ya kucheza mechi sita imekusanya pointi saba na safu ya ushambuliaji imefunga mabao matano.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, amesema kuwa masuala ambayo yanahusu usajili wowote ule ni suala la benchi la ufundi.
“Kwa namna ambavyo Azam FC tunafanya kazi kila kitengo kinatimiza wajibu wake kwa mfano linapokuja suala la usajili hapo ni benchi la ufundi wao wanapendekeza wachezaji ambao wanahitaji kisha uongozi unafanya jitihada za kuweza kuona wanaweza kujiunga na timu,”amesema Thabit.
Dirisha dogo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu na kufungwa Januari 16,2021 ambapo kwa mabosi wa Azam FC wanatajwa kuingia sokoni kusaka nyota wapya ambao wataimarisha kikosi hicho.