KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco, raia wa Hispania, amefichua malengo yao makubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanawaondoa wapinzani wao katika Kombe la Shirikisho Afrika, Red Arrows ya Zambia kutokana na maandalizi makubwa wanayoyafanya kwa sasa.
Simba inatarajia kucheza na Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Pablo ametoa kauli hiyo kuelekea mchezo wa kwanza wa kimataifa tangu ajiunge na timu hiyo, akichukua mikoba ya Didier Gomes Da Rosa, raia wa Ufaransa, ambaye aliachia ngazi baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pablo amesema kuwa anachokiangalia kwa sasa ni kuona wanafanikiwa kupita kwenye hatua hiyo kwenda makundi kwa kuwa ndiyo malengo yaliyosababisha wafanye maandalizi mazito ili kushinda mchezo huo.
“Tunaenda kwenye mchezo mgumu lakini matarajio yetu ni kupata matokeo mazuri kutokana na maandalizi ambayo tumekuwa tukiendelea nayo kabla ya kuelekea Zambia katika mchezo wa marudiano.
“Wapinzani wetu siyo wabaya na tunapaswa kuwaheshimu lakini kitu kikubwa ambacho tunakiangalia ni kwa jinsi gani tunaweza kutengeneza matokeo makubwa hapa ili iwe rahisi kwetu kufuzu kwenda katika hatua ya makundi, jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wetu,” amesema Pablo.