RED ARROWS WAPINZANI WA SIMBA WANA MCHECHETO

WAPINZANI wa Simba katika Kombe la Shirikisho barani Afrika, Klabu ya Red Arrows imeweka wazi kuwa nia yao ya kusonga mbele katika michuano hiyo huku wakitamba kufanya vizuri wakiwa ugenini.


Red Arrows kutoka Zambia Jumapili 
Novemba 28 watacheza mchezo wao wa kwanza wa mtoano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.


Mchezo wa marudiano unatarajiwa 
kufanyika Desemba Mosi nchini Zambia ambapo Simba watakuwa ugenini kuwakabili Red Arrows ambao watakuwa wenyeji.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Red Arrows, Chisi Mbewe alisema kuwa malengo yao ni kuhakikisha kuwa wanasonga mbele kwenda katika hatua inayofuata dhidi ya Simba licha ya kujua wanakutana na timu ngumu ambayo ina uzoefu wa mashindano ya kimataifa.


“Tunakwenda kupambana na Simba, 
tunatambua ubora wao na uzoefu mkubwa katika mashindano haya ya kimataifa hivyo lazima tupambane ili tuweze kuyafikia malengo yetu ambayo ni kufuzu kwenda katika hatua inayofuata ya michuano hii.


“Kila kitu ni malengo, kama 
tutafanikiwa kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza tukiwa ugenini basi naamini tutaimaliza mechi vizuri tukiwa nyumbani, muhimu ni kupambania tu malengo kama ambavyo sisi tutafanya,” alisema kocha huyo

KUTUA IJUMAA
Uongozi wa timu ya Red Arrows 
umeweka wazi kuwa wanatarajia kuwasili nchini usiku wa siku ya Ijumaa tayari kwa mchezo huo dhidi ya Simba.Meneja wa timu hiyo, Rio Flowers alisema: “Tupo kwenye maandalizi ya mwisho ya kujiandaa kuja huko kwa ajili ya mchezo wetu.

 

Safari yetu ya kuja huko tunategemea itakuwa siku ya Ijumaa ingawa bado sijajua itakuwa ni saa ngapi lakini kuna uwezekano wa kuingia huko usiku, jambo kubwa ni kwa wachezaji wetu kuweza kuendana na hali ya hewa ya huko japo kuwa haitofautiani na ile hapa kwetu.