IMEKUWA ni mwanzo mbaya kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye anga za kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mchezo wa kwanza imepoteza dhidi ya Horoya.
Simba ambao wapo kundi C walikuwa wana kazi ugenini dhidi ya Horoya ambao nao walikuwa wanahitaji matokeo na tumeona namna ilivyokuwa hasa kwenye matumizi ya nafasi.
Katika anga la kimataifa huku hakuna suala la kupoteza muda bali kila nafasi ni dhahabu inapaswa kutumiwa kwa umakini kwenye kutafuta pointi.
Malengo makubwa ambayo kila mmoja anayo ndani ya timu hayatatimia ikiwa kutakuwa hakuna matumizi mazuri ya nafasi kwenye mechi ambazo zinachezwa.
Hata wapinzani nao ambao walipata ushindi ni nafasi tatu za dhahabu walipata na kwenye hizo walitumia moja hivyo licha ya kushinda bado nao walikwama kutumia nafasi.
Kwa maana hiyo kwa uzoefu ambao Simba wanao ni wakati wao wa kuchanga karata upya ili kupata matokeo kwenye mechi zijazo.
Ikiwa watashindwa kubadili mwendo basi ngoma itakuwa ni nzito kwao kutusua hatua ya robo fainali kutokana na ushindani namna ulivyo.
Inawezekana kupata matokeo kwenye mechi zinazokuja lakini ni lazima wabadilike kwenye matumizi ya nafasi na kucheza kwa kushambulia huku wakijilinda.
Kasi inatakiwa iwe mwanzo mwisho wa mchezo sio ikifika kipindi cha pili wakati mchezo unakaribia kugota mwisho purukushani zinaanza hilo linapaswa kufanyiwa kazi.
Yanga pia kwenye mchezo wao dhidi ya US Monastir walipoteza pia ikiwa ni mchezo wa kwanza kwenye hatua ya makundi.
Kwenye mechi zijazo tunaamini kwamba benchi la ufundi litafanyia kazi makosa ambayo yamejitokeza kwenye mechi zao.