RAIS wa heshima wa Klabu ya Simba Mohammed Dewji amezungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi na viongozi walioongozana na timu hiyo nchini Dubai.
Hayo yote ameyafanya baada ya kuitembelea kambi ya Simba ya mazoezi nchini Dubai ambapo amepata nafasi ya kuongea na wachezaji na benchi la ufundi.
Miongoni mwa mambo ambayo amezungumza Mo ni kuhusu mipango ya kuhakikisha Simba inatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ipo kwenye hatua ya makundi Afrika ikiwa pamoja na timu ya Vipers iliyokuwa inanolewa na kocha ambaye kwa sasa yupo ndani ya kikosi hicho.
Ni Mo mwenyewe amehusika katika kuipeleka timu Dubai kwa kambi ya muda wa siku saba ili kumpa nafasi kocha mpya Roberto Oliviera raia wa Brazil kupata nafasi kusuka kikosi upya akishirikiana na Juma Mgunda.
Pia Mo amewashukuru mashabiki na Mtendaji Mkuu aliyeomba kujiuzulu na ataachia ngazi rasmi mara baada ya uchaguzi mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez.
Ikiwa nchini Dubai itacheza mechi mbili za kirafiki itakuwa dhidi ya Al Dhafra FC Januari 13 na CSKA Moscow itakuwa Januari 15 saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.