YANGA YAZIPIGIA HESABU POINTI ZA NAMUNGO

UONGOZI wa Yanga umebainisha kwamba unahitaji pointi tatu za Namungo kwenye mchezo wa leo Novemba 20 licha ya kwamba utakuwa ni mchezo mgumu.

Ikiwa ni namba moja kwenye msimamo na pointi zake 15 baada ya kucheza mechi tano ina kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Namungo FC.

Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amesema kuwa mkakati namba moja wa Yanga ni kutwaa ubingwa na haitawezekana ikiwa watashindwa kupata matokeo.

“Mradi namba moja ni kutwaa ubingwa wa ligi sasa haiwezi kutokea ikiwa tutashindwa kupata pointi tatu kwenye mechi ambazo tutacheza.

“Tumemaliza mechi tano kwa mafanikio hivyo kuelekea mchezo wetu wa sita dhidi ya Namungo ni lazima tuendelee kusaka pointi tatu. Namungo ni timu nzuri lakini tupo tayari.

“Mashabiki kwa namna ambavyo wamekuwa pamoja nasi na kwa mapokezi makubwa na mazuri basi tunaamini kwamba tutakuwa nao kila wakati wazidi kuwa pamoja nasi bila kuogopa,” amesema.

Yanga leo inatarajia kukosa huduma ya kiungo wake Khalid Aucho, Mapinduzi Balama na Dickson Ambundo ambao hawa hawapo fiti kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 waliopata dhidi ya Ruvu Shooting na watupiaji wakiwa ni Feisal Salum, Djuma Shaban na Tonombe Mukoko huku lile la Ruvu Shooting mtupiaji akiwa ni Shaban Msala.