YANGA WATAJA SABABU YA KUWAWAHI WAARABU

MAPEMA leo kikosi cha Yanga kimeanza safari kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuwakabili wapinzani wao Club Africain.

Jesus Moloko nyota wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye msafara ulioanza safari leo Novemba 4,2022 kuelekea nchini Tunisia.

Bernard Morrison, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Diara, Mshery, Kibwana Shomari na Dickson Job nao wapo kwenye msafara huo pia.

Yanga ina kibarua cha kwenda kusaka ushindi kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho nchini Tunisia ukiwa ni mchezo wa pili.

Ule wa awali uliochezwa Uwanja wa Mkapa, ubao ulisoma Yanga 0-0 Club Africain hivyo kibarua kwa Yanga ni kusaka ushindi wa aina yoyote ama sare ya kufungana.

Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo jambo ambalo limewafanya wawahi kuelekea ugenini kufanya maandaalizi ya mwisho.

“Tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini wachezaji wapo tayari na ndio maana tumewahi ili kufanya maandalizi muhimu kuelekea kwenye mchezo wetu,” amesema.