MAKIPA WALIOPATA TABU MBELE YA FEI TOTO

KWENYE ardhi ya Tanzania mbali na uzuri wa mlima Kilimanjaro pamoja na wakazi wake wenye sifa ya upole na ukarimu kuna kijana anakiwasha kwenye ulimwengu wa soka kwa kufanya kazi ya mpira ionekane kuwa nyepesi.

Jina lake anaitwa Feisal Salum wengi wanapenda kumuita Fei Toto ni kijana anayewapa tabu kwa sasa makipa wa Bongo kwa mabao yake yenye ujazo wa kutosha licha ya mwili wake kuwatofauti na kile ambacho anakifanya.

Ikiwa ni msimu wa 2021/22 akiwa anakipiga ndani ya Yanga kwa sasa Fei Toto ni nyota namba moja kwenye utupiaji wa mabao akiwa nayo matatu kibindoni.

Yanga ikiwa imecheza jumla ya mechi tano na kutupia mabao 9 yeye amehusika kwenye mabao manne akiwa amefunga mabao matatu na pasi moja ya bao ambayo alimpa mshikaji wake Fiston Mayele.

Gumzo kubwa kwake ni kutokana na mtindo wa ufungaji wake wa mabao ambao haujawa rafiki kwa makipa wengi hapa leo tunakuletea baadhi ya makipa aliowapa tabu kwa mabao yake jambo ambalo linawafanya wamkumbuke mara kwa mara:-

Juma Kaseja

Kipa namba moja wa KMC ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo anaingia kwenye orodha ya makipa walioteswa na mabao ya Fei Toto.

Ilikuwa Oktoba 25/2018 Uwanja wa Mkapa wakati huo Kocha Mkuu alikuwa ni Mwinyi Zahera katulia zake benchi anasoma mchezo unakwendaje.

Heritier Makambo alichezewa faulo nje kidogo ya 18 na All Ally na kwa kitendo hicho alionyeshwa kadi ya njano na kazi ya kupiga faulo alipewa Fei Toto.

Mguu wa kulia ulimuadhibu Kaseja ambaye hakuwa na chaguo la kufanya ilikuwa ni dakika ya 89 na ubao wa Uwanja wa Mkapa ukasoma KMC 0-1 Yanga.

Deogratius Munish, ‘Dida’

Akiwa na Ihefu FC msimu wa 2020/21 hakuwa na bahati ya kuinusuri timu hiyo ishindwe kushuka daraja kwa kuwa miguu ya Fei Toto ilimpa tabu kwa kumtungua mabao mawili akiwa hana la kufanya.

Mabao hayo Fei Toto aliyafunga Uwanja wa Mkapa lile la kwanza alimtungua dakika ya 17 na bao la pili alimtungua dakika ya 36 na alipiga mashuti hayo akiwa ndani ya 18.

Pia Fei Toto aliwatungua Ihefu, Desemba 23 walipokutana Uwanja wa Sokoine Mbeya na kipa alikuwa ni Dida mwenyewe langoni.

Bidii Hussein

Wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa unasoma Ruvu Shooting 2-3 Yanga langoni alikuwa amekaa Bidii Hussein ambapo aliokoteshwa mabao mawili na Feitoto na yote alitumia mguu wake wa kushoto yaliyompa tabu kipa huyo licha ya kuonesha bidii alikwama kuyaokoa yalizama nyavuni ilikuwa ni dakika ya 22 na 31.

Farouk Shikalo

Kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Majimaji, Songea, Fei Toto alipachika bao bora akiwa nje ya 18 ilikuwa ni Oktoba 19. Kwenye mchezo huo Fei alikuwa ni nyota wa mchezo kwa kuwa alifunga na kutoa pasi ya bao kwa Mayele.

Mohamed Makaka

Alikuwa shujaa kwenye mchezo uliochezwa Novemba 2 kwa kuokoa michomo 7 ya mshambuliaji Fiston Mayele ila alikwama kuokoa mchomo mmoja wa Feisal Salum ambaye alifungua njia kisha wengine wakafuata wakati Yanga iliposhinda mabao 3-1.

Bao lake lenye ujazo nje ya 18 liliwafanya mashabiki wasiamini wanachokiona huku Makaka naye akiweka wazi kwamba hakuwa na chaguo la kufanya.

Neno la Feisal

“Kufunga mabao ya aina ile kwangu naona ni kawaida tu nab ado nitaendelea kufuanga sana kwa sababu ninapenda kuipa ushindi timu na ni vitu ambavyo huwa ninavifanyia mazoezi,”.