ANDORRA, HISPANIA – Mmiliki wa klabu ya FC Andorra, Gerard Pique, amepinga adhabu ya kufungiwa mechi 12 aliyopewa kipa wa timu hiyo, Jesus Owono, kufuatia tukio la kugongana na mshambuliaji wa CD Tenerife, Jesus de Miguel, aliyefariki dunia siku moja baada ya mechi hiyo.
De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alifariki Novemba 3, 2026, baada ya kupata matatizo ya moyo yaliyosababisha moyo wake kusimama, kufuatia tukio la kugongana na Owono wakati wa mchezo wa ligi daraja la pili nchini Hispania Novemba 2.
Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) ilimfungia Owono mechi 12 kwa kosa la kucheza kwa vitendo vya vurugu vilivyosababisha majeraha makubwa.
Hata hivyo, Pique, ambaye ni nyota wa zamani wa Barcelona, amesema kipa huyo hakustahili adhabu hiyo kubwa kwa kuwa tukio lililotokea lilikuwa ajali na si kitendo cha makusudi.
Akizungumza kupitia video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu usiku, Pique alisema wachezaji, makocha na makipa mbalimbali wamekuwa wakilitambua tukio hilo kama ajali.
Pique alieleza kuwa kumpa Owono adhabu ya juu zaidi katika mazingira hayo kunamweka katika hali ambayo haistahili, akisisitiza kuwa kipa huyo hana lawama ya moja kwa moja kwa matokeo ya kusikitisha yaliyotokea.
Katika kutetea hoja yake, Pique alilinganisha tukio hilo na adhabu ya mechi tatu aliyopewa Jose Corpas wa Albacete baada ya kumkanyaga kwa bahati mbaya kichwani mchezaji wa Sabadell, Quadri Liameed, katika mchezo mwingine wa Hispania.
Alisema tofauti kubwa kati ya matukio hayo ni kwamba Liameed aliendelea kuwa hai na kupona, wakati De Miguel alipoteza maisha.
Kutokana na hali hiyo, Pique alihoji iwapo kamati ya nidhamu inapopanga adhabu inapaswa kuzingatia kitendo kilichofanyika au matokeo yaliyotokana na tukio hilo.
Hadi wakati wa taarifa hiyo, Shirikisho la Soka la Hispania halikuwa limetoa majibu kuhusu maoni ya Pique.
Wakati huohuo, Owono mwenye umri wa miaka 25 amejiondoa katika kikosi cha timu ya taifa ya Equatorial Guinea kilichojiandaa kucheza mechi za kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Zimbabwe mwezi huu.
Pique pia alisema kuna uwezekano kipa huyo akahitaji muda mrefu zaidi kurejea uwanjani hata baada ya kumaliza adhabu yake ya mechi 12, kutokana na athari za tukio hilo.
Alisisitiza kuwa hakuna adhabu yoyote itakayoweza kumrudisha De Miguel katika maisha.