Dladla Atoa Onyo kwa Wachezaji wa Yanga, Asema Wanadaiwa Soka Zuri

Kocha wa muda wa Yanga, Simon Dladla, leo Oktoba 26, 206 amekiri kuwa timu hiyo ina deni kubwa kwa mashabiki wake kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika mchezo uliopita, akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kurejesha furaha kwa Wananchi.

Dladla amesema Yanga inahitaji kuwa makini zaidi katika kutumia nafasi za kufunga mabao, hasa inapocheza nyumbani, akisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kuwa wakali na kufanya maamuzi ya haraka na sahihi mbele ya lango la wapinzani.

“Tunacheza nyumbani, hivyo ni lazima tuwe wakali na wenye maamuzi haraka na sahihi mbele ya lango. Tunapaswa kutumia vizuri nafasi zetu na kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyahitaji. Sisi ni wataalamu wa mchezo huu na tunaelewa changamoto zinazotukabili. Ninaamini tuko tayari,” amesema Dladla.

Kocha huyo ameeleza kuwa jukumu kubwa la kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri lipo mikononi mwa wachezaji, huku akibainisha kuwa mabadiliko ya kimfumo na kimbinu yatategemea wachezaji watakaokuwepo kwa ajili ya mchezo unaofuata.

Amesema benchi la ufundi linaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza, likiwa na lengo la kuifanya Yanga icheze soka la kuvutia na kurejea katika ushindani unaoendana na matarajio ya klabu hiyo.

“Malengo makubwa ya Yanga ni kuhakikisha tunakuwa namba moja,” amesema Dladla.

Akizungumzia matokeo ya mchezo uliopita, Dladla amekiri kuwa kikosi hicho kiliwaangusha mashabiki wake kwa kushindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa, lakini amewataka Wananchi kuendelea kuwa na imani na timu yao.

Amesema wachezaji na benchi la ufundi wanafahamu matarajio ya mashabiki, hivyo wanapaswa kuonyesha mwitikio ndani ya uwanja kwa kupata matokeo mazuri, kufunga mabao na kuonyesha kiwango cha juu cha ushindani.

“Kwa Wananchi, tunafahamu kuwa tuliwakatisha tamaa katika mchezo uliopita kwa sababu hatukupata matokeo tuliyokuwa tunayatarajia. Tumeyatambua mapungufu yetu na tutafanya kazi kwa bidii. Tunafahamu kuwa tuna deni kubwa kwenu. Tunadaiwa magoli, tunadaiwa soka zuri na kiwango cha juu cha ushindani kila tunaposhuka uwanjani,” amesema Dladla.

Aidha, kocha huyo amewaomba mashabiki wa Yanga kuipa benchi la ufundi na wachezaji muda wa kufanya kazi, huku akiwataka kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuendelea kukipa nguvu kikosi hicho.

Amesisitiza kuwa timu itapambana kuhakikisha inapata matokeo yatakayorejesha tabasamu kwa mashabiki wake na kuwapa sababu ya kuendelea kuiamini klabu yao.

Mshery aonya kuhusu ugumu wa mchezo dhidi ya Mashujaa

Kwa upande wake, mchezaji wa Yanga, Aboutwaleeb Mshery, amesema mchezo unaofuata dhidi ya Mashujaa hautakuwa rahisi kutokana na ushindani ambao wapinzani hao wamekuwa wakiutoa katika ligi ya Tanzania.

Mshery amesema pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza, wachezaji wa Yanga wanapaswa kupambana kwa juhudi zote ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

“Hautakuwa mchezo rahisi kwa namna ambavyo Mashujaa wanacheza. Ni timu ambayo imekuwa ikitoa ushindani mkubwa kwenye ligi. Nachoweza kuwahakikishia wachezaji ni kupambana kwa juhudi zote ili tupate matokeo mazuri,” amesema Mshery.

Ameeleza pia kuwa mabadiliko yaliyofanyika kwenye benchi la ufundi hayamaanishi kuwa timu imeanza upya kila kitu, akibainisha kuwa Dladla si mgeni kwa kikosi hicho na tayari anaifahamu ligi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Mshery, kocha huyo anaendelea kurekebisha changamoto zilizojitokeza ili kuandaa mazingira mazuri ya ushindi katika mchezo unaofuata.

Mshery: Sare ya Arusha haitabadilisha malengo ya Yanga
Mshery amesisitiza kuwa sare iliyopatikana Arusha haimaanishi kuwa Yanga imepoteza mwelekeo au malengo yake ya msimu huu, akieleza kuwa matokeo ya aina hiyo ni sehemu ya mchezo wa soka.

Amesema kila mmoja ndani ya klabu anatambua wajibu wake na umuhimu wa kuendelea kupambana licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza katika mbio za kuwania mafanikio.

“Kutoka sare Arusha hakumaanishi sisi tunapoteza malengo yetu. Kila mmoja wetu klabu hapa anajua nini cha kufanya. Sio mara ya kwanza kwa Yanga kupata sare. Ni sehemu ya mchezo wa soka. Nyakati kama hizi hutokea lakini sio za kudumu. Uimara na umoja wetu ndio utaamua hatma yetu msimu huu. Yaliyopita yamepita sasa tunapambana kwa yanayokuja,” amesema Mshery.

Kauli za Dladla na Mshery zinaashiria dhamira ya Yanga kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza, kuongeza ufanisi wa safu ya ushambuliaji na kurejesha imani ya mashabiki wake kupitia kiwango bora na matokeo chanya katika michezo inayofuata.